Danieli 7:2-4
Danieli 7:2-4 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mimi Danieli niliona katika maono usiku, pepo nne toka pande zote za mbinguni zikiichafua bahari kuu. Wanyama wakubwa wanne, wakainuka kutoka humo baharini, kila mmoja tofauti na mwenzake. Mnyama wa kwanza alikuwa kama simba, na alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikiwa namwangalia, mabawa yake yalingolewa, naye akainuliwa na kusimama kwa miguu miwili kama binadamu. Kisha, akapewa akili ya binadamu.
Danieli 7:2-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Danieli akanena, akisema, Niliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa. Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali. Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake akanyonyoka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu.
Danieli 7:2-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa. Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali. Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake yakafutuka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu.
Danieli 7:2-4 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, na hapo mbele yangu kulikuwa na pepo kutoka pande nne za mbingu, zikivuruga bahari kuu. Wanyama wanne wakubwa, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka bahari. “Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa ya tai. Nikatazama hadi mabawa yake yalipongʼolewa, naye akainuliwa katika nchi, akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.