Danieli 7:1-25
Danieli 7:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa mfalme Belshaza wa Babuloni, Danieli aliota ndoto na kuona maono akiwa amelala kitandani mwake. Aliiandika ndoto yake hii: “Mimi Danieli niliona katika maono usiku, pepo nne toka pande zote za mbinguni zikiichafua bahari kuu. Wanyama wakubwa wanne, wakainuka kutoka humo baharini, kila mmoja tofauti na mwenzake. Mnyama wa kwanza alikuwa kama simba, na alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikiwa namwangalia, mabawa yake yalingolewa, naye akainuliwa na kusimama kwa miguu miwili kama binadamu. Kisha, akapewa akili ya binadamu. “Mnyama wa pili alikuwa kama dubu ambaye upande wake mmoja ulikuwa umeinuka. Kinywani mwake alikuwa na mbavu tatu alizozishikilia kwa meno yake. Sauti ikamwambia, ‘Haya, kula nyama nyingi kadiri uwezavyo.’ “Baada ya hayo, nilimwona mnyama mwingine. Huyu alikuwa kama chui mwenye mabawa manne ya ndege mgongoni mwake. Alikuwa na vichwa vinne na alipewa mamlaka. “Kisha, katika maono yangu hayo ya usiku nikamwona mnyama wa nne wa ajabu na wa kutisha, mwenye nguvu sana. Huyu alikuwa na meno makubwa ya chuma ambayo aliyatumia kula na kuvunjavunja, na mabaki aliyakanyagakanyaga kwa nyayo zake. Alikuwa tofauti na wale wanyama wengine watatu, kwani alikuwa na pembe kumi. Nilipokuwa naziangalia hizo pembe, niliona upembe mwingine mdogo ukiota miongoni mwa zile kumi. Ili kuupa nafasi upembe huu zile pembe nyingine tatu zilingolewa pamoja na mizizi yake. Ulikuwa na macho ya binadamu na kinywa kilichotamka maneno ya kujigamba. “Nikiwa bado naangalia, viti vya enzi viliwekwa hapo, kisha ‘Mzee wa kale na kale’ akaja, akaketi. Alikuwa amevaa vazi jeupe kama theluji; nywele zake zilikuwa kama sufu safi. Kiti chake cha enzi kilikuwa cha miali ya moto na magurudumu ya kiti chake yalikuwa ya moto uwakao. Kutoka kiti hicho kijito cha moto kilibubujika, kikatiririka. Maelfu walimtumikia, na mamilioni walisimama mbele yake. Mahakama ikawa tayari kwa kikao, na vitabu vikafunguliwa. “Kutokana na maneno ya kujigamba yaliyokuwa yanasemwa na ile pembe, nikatazama. Nikiwa natazama, huyo mnyama wa nne aliuawa, mwili wake ukaharibiwa na kutolewa uchomwe moto. Wale wanyama wengine walinyanganywa mamlaka yao, lakini wao wenyewe wakaachwa waendelee kuishi kwa muda fulani. “Wakati wa maono haya usiku, niliona mmoja kama mwana wa mtu akija katika mawingu, akamwendea yule ‘Mzee wa kale na kale,’ wakanileta mbele yake. Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme, ili watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote wamtumikie. Utawala wake ni wa milele na ufalme wake kamwe hautaangamizwa. “Maono niliyoyaona mimi Danieli yalinishtua, nami nikafadhaika. Nilimkaribia mmojawapo wa wale waliosimama huko na kumwuliza maana halisi ya mambo hayo yote. Naye akanisimulia na kunieleza maana yake: ‘Wanyama hao wanne wakubwa ni wafalme wanne watakaotokea duniani. Lakini watakatifu wa Mungu Mkuu watapewa ufalme, nao wataumiliki ufalme huo milele na milele.’ “Kisha nikataka nielezwe juu ya yule mnyama wa nne, ambaye alikuwa tofauti kabisa na wale wengine, wa ajabu na wa kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma na makucha yake ya shaba. Aliyatumia meno hayo kula na kuvunjavunja, na mabaki aliyakanyagakanyaga kwa nyayo zake. Aidha nilitaka nielezwe juu ya zile pembe kumi alizokuwa nazo kichwani mwake, na ule upembe mmoja ambao kabla haujaota, zilingoka pembe tatu; upembe uliokuwa na macho na kinywa ambacho kilitamka maneno ya kujigamba, na ambao ulionekana kuwa mkubwa kuliko pembe nyingine. “Nikiwa bado naangalia, pembe hiyo ilipigana vita na watakatifu, nayo ikawashinda. Lakini yule ‘Mzee wa kale na kale’ akainuka, akawapa haki watakatifu wa Mungu na wakati ulipotimia, hao watakatifu wakapewa ufalme. “Nikaelezwa hivi: ‘Yule mnyama wa nne ni ufalme wa nne utakaokuwako duniani. Ufalme huo utakuwa tofauti na falme nyingine, nao utaiangamiza dunia nzima. Utaibwaga chini na kuipasua vipandevipande. Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huo. Halafu watafuatwa na mfalme mwingine ambaye atakuwa tofauti na wale waliomtangulia, na atawaangusha wafalme watatu. Huyo atamkufuru Mungu Mkuu na kuwatesa watakatifu wake. Atajaribu kubadilisha nyakati na sheria zao, na watakatifu watatiwa mikononi mwake kwa muda wa miaka mitatu na nusu.
Danieli 7:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danieli alipata ndoto, na maono kichwani nwake, akiwa kitandani mwake; kisha akaiandika hiyo ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo. Danieli akanena, akisema, Niliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa. Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali. Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake akanyonyoka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu. Na tazama, mnyama mwingine, wa pili, kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake; wakamwambia mnyama huyo hivi, Inuka, ule nyama tele. Kisha nikatazama, na kumbe! Mnyama mwingine, kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka. Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mnyama wa nne, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi. Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang'olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu. Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu wakamtumikia, na mamilioni wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikatazama wakati huo; kwa sababu ya sauti ya yale maneno makubwa iliyoyasema ile pembe; nilitazama hata mnyama yule akauawa, mwili wake ukaharibiwa, akatolewa ateketezwe kwa moto. Na kwa habari za wale wanyama wengine, walinyang'anywa mamlaka yao; lakini maisha yao yalidumishwa kwa wakati na majira. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. Basi, mimi Danieli, roho yangu ilihuzunika ndani yangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha. Nikamkaribia mmoja wa hao waliosimama karibu, nikamwuliza maana ya kweli ya hayo yote. Basi akaniambia, akanijulisha tafsiri ya mambo hayo. Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wanne watakaotokea duniani. Lakini watakatifu wake Aliye Juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam hata milele na milele. Kisha nilitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kinywa kilichonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake Aliye Juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme. Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utaangamiza dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande. Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu. Naye atanena maneno kinyume chake Aliye Juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye Juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa nyakati tatu na nusu
Danieli 7:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danieli aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo. Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa. Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali. Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake yakafutuka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu. Na tazama, mnyama mwingine, wa pili, kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake; wakamwambia mnyama huyo hivi, Inuka, ule nyama tele. Kisha nikatazama, na kumbe! Mnyama mwingine, kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka. Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mnyama wa nne, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi. Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang’olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu. Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikatazama wakati huo; kwa sababu ya sauti ya yale maneno makubwa iliyoyasema ile pembe; nalitazama hata mnyama yule akauawa, mwili wake ukaharibiwa, akatolewa ateketezwe kwa moto. Na kwa habari za wale wanyama wengine, walinyang’anywa mamlaka yao; walakini maisha yao yalidumishwa kwa wakati na majira. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. Basi, mimi Danieli, roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha. Nikamkaribia mmoja wa hao waliosimama karibu, nikamwuliza maana ya kweli ya hayo yote. Basi akaniambia, akanijulisha tafsiri ya mambo hayo. Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wanne watakaotokea duniani. Lakini watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam hata milele na milele. Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme. Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande. Na habari za zile pembe kumi, katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu. Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.
Danieli 7:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Belshaza mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, nayo maono yakapita mawazoni mwake alipokuwa amelala kitandani mwake. Akayaandika mambo aliyoyaona katika ndoto yake. Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, na hapo mbele yangu kulikuwa na pepo kutoka pande nne za mbingu, zikivuruga bahari kuu. Wanyama wanne wakubwa, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka bahari. “Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa ya tai. Nikatazama hadi mabawa yake yalipongʼolewa, naye akainuliwa katika nchi, akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu. “Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, aliyefanana na dubu. Upande wake mmoja alikuwa ameinuka, na alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama, ushibe!’ “Baada ya huyo, nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala. “Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, na mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya, tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma; akapondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chini ya nyayo zake chochote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi. “Nilipokuwa nikifikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ndogo, iliyojitokeza miongoni mwa zile kumi; pembe tatu za mwanzoni zilingʼolewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu, na mdomo ulionena kwa majivuno. “Nilipoendelea kutazama, “viti vya utawala vikawekwa, naye Mzee wa Siku akaketi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji; nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama sufu. Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka miali ya moto, nayo magurudumu yake yote yalikuwa yanawaka moto. Mto wa moto ulikuwa unatiririka, ukipita mbele yake. Maelfu elfu wakamhudumia; kumi elfu mara kumi elfu wakasimama mbele zake. Mahakama ikakaa kuhukumu, na vitabu vikafunguliwa. “Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia hadi yule mnyama alipouawa, na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto uliowaka. (Wanyama wengine walikuwa wamevuliwa mamlaka yao, lakini waliruhusiwa kuishi kwa muda.) “Katika maono yangu ya usiku nilitazama, na mbele yangu nikamwona mtu kama Mwana wa Adamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku, na akaongozwa mbele zake. Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu; nao watu wa makabila yote, na mataifa, na wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa. “Mimi Danieli nilipata mahangaiko rohoni, nayo maono yale yaliyopita ndani ya mawazo yangu yalinisumbua. Nikamkaribia mmoja wa wale waliosimama pale, nikamuuliza maana halisi ya haya yote. “Basi akaniambia na kunipa tafsiri ya vitu hivi: ‘Hao wanyama wanne wakubwa ni falme nne zitakazoinuka duniani. Lakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele: naam, milele na milele.’ “Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, aliyekuwa tofauti na wale wengine wote, tena wa kutisha sana, na meno yake ya chuma na makucha ya shaba: mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake, na kukanyaga chochote kilichosalia. Pia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake, na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho kuliko zile nyingine, na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno. Nilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda, hadi huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipoumiliki ufalme. “Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote, nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda. Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu. Atanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwatesa watakatifu wake, huku akijaribu kubadili majira na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati.