Danieli 6:13-23
Danieli 6:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakamwambia mfalme, “Yule Danieli aliye mmoja wa mateka kutoka nchi ya Yuda hakuheshimu wewe mfalme wala haitii amri uliyotia sahihi. Yeye anasali mara tatu kila siku.” Mfalme aliposikia maneno hayo, alisikitika sana. Akajitahidi sana kupata njia ya kumwokoa Danieli. Aliendelea kujaribu mpaka jua likatua. Wale watu wakamwendea mfalme Dario kwa pamoja na kumwambia, “Ee mfalme, ujue kuwa hakuna sheria wala amri yoyote ya Wamedi na Wapersi inayoweza kubatilishwa baada ya kuwekwa na mfalme.” Ndipo mfalme Dario akatoa amri, naye Danieli akaletwa na kutupwa katika pango la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako ambaye unamtumikia daima, na akuokoe.” Jiwe likaletwa na kuwekwa mlangoni mwa lile pango. Mfalme akalipiga mhuri wake binafsi na ule wa wakuu wake, ili uamuzi kuhusu Danieli usibatilishwe. Kisha mfalme akarudi katika ikuluni yake ambamo alikesha akifunga; hakufanya tafrija ya aina yoyote, na usingizi ukampaa. Alfajiri na mapema, mfalme Dario aliamka, akaenda kwa haraka kwenye pango la simba. Alipofika karibu akamwita Danieli kwa sauti ya huzuni, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai! Je, Mungu wako unayemtumikia daima ameweza kukuokoa na simba hawa?” Danieli akamjibu mfalme, “Uishi, ee mfalme! Mungu wangu alileta malaika wake kuvifumba vinywa vya simba hawa, nao hawakunidhuru. Alifanya hivyo kwa sababu alijua mimi sina lawama yoyote kwake na wala sijafanya lolote baya mbele yako.” Hapo mfalme akafurahi sana; akaamuru Danieli atolewe pangoni. Basi wakamtoa, naye alikuwa hajadhurika hata kidogo, kwa sababu alimtegemea Mungu wake.
Danieli 6:13-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lolote lililo marufuku, wala amri yoyote iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia mhuri kwa mhuri wake mwenyewe, na kwa mhuri wa wakuu wake, lisibadilike neno lolote katika habari za Danieli. Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye amevifunga vinywa vya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nilionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala halikuonekana dhara lolote mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake.
Danieli 6:13-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku. Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa. Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli. Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake.
Danieli 6:13-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo wakamwambia mfalme, “Danieli, ambaye ni mmoja wa mahamisho kutoka Yuda, hakuheshimu, ee mfalme, wala hajali amri uliyoiweka kwa maandishi. Bado anaomba mara tatu kwa siku.” Mfalme aliposikia hili, akahuzunika mno. Akakusudia kumwokoa Danieli, hivyo akafanya kila jitihada ya kumwokoa hadi jua likatua. Ndipo wale watu wakamwendea mfalme kama kikundi na kumwambia, “Ee mfalme, kumbuka kwamba kulingana na sheria ya Wamedi na Waajemi, hakuna amri wala sheria ambayo mfalme ameitoa inayoweza kubadilishwa.” Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa ndani ya tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako unayemtumikia daima na akuokoe!” Jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mlango wa tundu, naye mfalme akalitia muhuri kwa pete yake mwenyewe pamoja na kwa pete za wakuu wake, ili hali ya Danieli isiweze kubadilishwa. Kisha mfalme akarudi kwenye jumba lake la kifalme, naye usiku kucha hakuweza kula wala kutumia viburudisho alivyoletewa, na hakuweza kulala. Asubuhi na mapema, mfalme akaondoka na kuharakisha kwenda kwenye tundu la simba. Alipokaribia lile tundu, mfalme akamwita Danieli kwa sauti ya uchungu: “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai! Je, Mungu wako, unayemtumikia daima, ameweza kukuokoa kwa simba?” Danieli akajibu, “Ee mfalme, uishi milele! Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lolote baya mbele yako, ee mfalme.” Basi Mfalme akafurahi mno, akatoa amri Danieli atolewe kutoka kwa lile tundu. Danieli alipotolewa kutoka kwa lile tundu, hakukutwa na jeraha lolote, kwa sababu alikuwa amemtumaini Mungu wake.