Danieli 5:1-6
Danieli 5:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja mfalme Belshaza aliwaandalia karamu kubwa maelfu ya wakuu wake na kunywa divai pamoja nao. Kutokana na kunywa divai, mfalme Belshaza akatoa amri vile vyombo vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza, baba yake, alivichukua kutoka hekalu la Yerusalemu, viletwe ili avitumie kunywea divai pamoja na maofisa wake, wake zake na masuria wake. Basi, vile vyombo vya dhahabu na fedha vilivyochukuliwa hekaluni Yerusalemu vikaletwa. Mfalme, maofisa wake, wake zake na masuria wake wakavitumia kunywea. Walikunywa huku wanaisifu miungu iliyotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, chuma, miti na mawe. Mara, vidole vya mkono wa mwanaadamu vikatokea na kuandika kwenye lipu ya ukuta wa ikulu ya mfalme, mahali palipomulikwa vizuri, mkabala na kinara cha taa. Mfalme aliuona mkono huo ukiandika. Basi, mfalme akabadilika rangi na fikira zake zikamfadhaisha, viungo vyake vikalegea na magoti yakaanza kutetemeka.
Danieli 5:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mfalme Belshaza, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya hao elfu. Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadneza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wapate kuvinywea. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe. Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokielekea kinara; naye mfalme akakiona kiganja cha ule mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.
Danieli 5:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Belshaza, mfalme, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya elfu hao. Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadreza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wapate kuvinywea. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe. Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.
Danieli 5:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mfalme Belshaza aliandaa karamu kubwa kwa ajili ya wakuu wake elfu moja, na akanywa mvinyo pamoja nao. Belshaza alipokuwa akinywa divai, aliamuru vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekalu huko Yerusalemu viletwe, ili mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wapate kuvinywea. Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wakavinywea. Walipokuwa wakinywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe. Ghafula vidole vya mkono wa mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya chokaa ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika. Uso wa mfalme ukageuka rangi, naye akaogopa sana, kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea.