Danieli 5:1-12
Danieli 5:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja mfalme Belshaza aliwaandalia karamu kubwa maelfu ya wakuu wake na kunywa divai pamoja nao. Kutokana na kunywa divai, mfalme Belshaza akatoa amri vile vyombo vya dhahabu na fedha ambavyo mfalme Nebukadneza, baba yake, alivichukua kutoka hekalu la Yerusalemu, viletwe ili avitumie kunywea divai pamoja na maofisa wake, wake zake na masuria wake. Basi, vile vyombo vya dhahabu na fedha vilivyochukuliwa hekaluni Yerusalemu vikaletwa. Mfalme, maofisa wake, wake zake na masuria wake wakavitumia kunywea. Walikunywa huku wanaisifu miungu iliyotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, chuma, miti na mawe. Mara, vidole vya mkono wa mwanaadamu vikatokea na kuandika kwenye lipu ya ukuta wa ikulu ya mfalme, mahali palipomulikwa vizuri, mkabala na kinara cha taa. Mfalme aliuona mkono huo ukiandika. Basi, mfalme akabadilika rangi na fikira zake zikamfadhaisha, viungo vyake vikalegea na magoti yakaanza kutetemeka. Mfalme Belshaza akapaaza sauti waletwe wachawi, Wakaldayo wenye hekima na wanajimu waletwe. Walipoletwa, mfalme akawaambia wenye hekima hao wa Babuloni, “Yeyote atakayesoma maandishi haya na kunijulisha maana yake, atavishwa mavazi rasmi ya zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, na kupewa nafasi ya tatu katika ufalme.” Basi, wenye hekima wote wa mfalme wakaja, lakini hawakuweza kuyasoma maandishi hayo wala kumjulisha mfalme maana yake. Basi, mfalme Belshaza akazidi kuhangaika na rangi yake ikazidi kugeuka, nao wakuu wake wakawa na wasiwasi. Kutokana na kelele za mfalme na wakuu wake, mama mfalme aliingia ukumbini mwa karamu, akasema, “Uishi, ee mfalme! Si lazima mawazo yako yakufadhaishe na kubadilika rangi yako. Katika ufalme wako yupo mtu ambaye roho ya miungu mitakatifu imo ndani yake. Wakati wa utawala wa baba yako, mtu huyu alidhihirika kuwa mwenye ujuzi, ufahamu na hekima kama ya miungu. Baba yako, mfalme Nebukadneza, alimfanya kuwa mkuu wa waaguzi, wachawi, Wakaldayo wenye hekima, na wanajimu, kwa sababu ana roho njema, maarifa, ujuzi wa kufasiri ndoto, kufumbua mafumbo na kutatua matatizo. Jina la mtu huyo ni Danieli ambaye baba yako alimwita Belteshaza. Basi na aitwe, naye atakueleza maana ya maandishi haya.”
Danieli 5:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mfalme Belshaza, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya hao elfu. Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadneza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wapate kuvinywea. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe. Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokielekea kinara; naye mfalme akakiona kiganja cha ule mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana. Mfalme akalia kwa sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko haya, na kunionesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika ufalme. Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake. Ndipo mfalme Belshaza akahangaika sana, uso wake ukambadilika, na wakuu wake wakaona fadhaa. Basi malkia, kwa sababu ya maneno ya mfalme na ya wakuu wake, akaingia katika nyumba ya karamu; malkia akanena, akasema, Ee mfalme, uishi milele; fikira zako zisikufadhaishe; wala uso wako usibadilike. Yuko mtu katika ufalme wako, ambaye roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yake; na katika siku za baba yako nuru na ufahamu na hekima zilionekana ndani yake; na mfalme Nebukadneza, baba yako, naam, mfalme, baba yako, akamfanya kuwa mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na kufungua mafundo, zilionekana katika Danieli huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danieli, naye ataionesha tafsiri.
Danieli 5:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Belshaza, mfalme, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya elfu hao. Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadreza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wapate kuvinywea. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe. Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana. Mfalme akalia kwa sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika ufalme. Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake. Ndipo mfalme Belshaza akahangaika sana, uso wake ukambadilika, na wakuu wake wakaona fadhaa. Basi malkia, kwa sababu ya maneno ya mfalme na ya wakuu wake, akaingia katika nyumba ya karamu; malkia akanena, akasema, Ee mfalme, uishi milele; fikira zako zisikufadhaishe; wala uso wako usibadilike. Yuko mtu katika ufalme wako, ambaye roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yake; na katika siku za baba yako nuru na ufahamu na hekima zilionekana ndani yake; na mfalme Nebukadreza, baba yako, naam, mfalme, baba yako, akamfanya kuwa mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na kufungua mafundo, zilionekana katika Danieli huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danieli, naye ataionyesha tafsiri.
Danieli 5:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mfalme Belshaza aliandaa karamu kubwa kwa ajili ya wakuu wake elfu moja, na akanywa mvinyo pamoja nao. Belshaza alipokuwa akinywa divai, aliamuru vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekalu huko Yerusalemu viletwe, ili mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wapate kuvinywea. Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, pamoja na wake zake na masuria wake wakavinywea. Walipokuwa wakinywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu na fedha, ya shaba, chuma, miti na mawe. Ghafula vidole vya mkono wa mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya chokaa ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika. Uso wa mfalme ukageuka rangi, naye akaogopa sana, kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea. Mfalme akawaita wasihiri, wanajimu na waaguzi waletwe, naye akawaambia hao wenye hekima wa Babeli, “Yeyote asomaye maandishi haya na kuniambia maana yake atavikwa nguo za zambarau, na kuvikwa mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atafanywa mtawala wa cheo cha tatu katika ufalme.” Ndipo wenye hekima wote wa mfalme wakaingia, lakini hawakuweza kusoma yale maandishi wala kumwambia mfalme maana yake. Basi Mfalme Belshaza akazidi kujawa na hofu, na uso wake ukageuka rangi zaidi. Wakuu wake wakapigwa na bumbuazi. Malkia aliposikia sauti za mfalme na wakuu wake, alikuja katika ukumbi wa karamu. Akasema, “Ee mfalme, uishi milele! Usishtuke! Usibadilike rangi hivyo! Yuko mtu katika ufalme wako mwenye roho ya miungu mitakatifu ndani yake. Wakati wa baba yako, mtu huyo alionekana kuwa na ufahamu, akili na hekima kama ile ya miungu. Mfalme Nebukadneza baba yako, naam, mfalme baba yako, alimweka kuwa mkuu wa waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi. Mtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza, alionekana kuwa na akili nyepesi, maarifa na ufahamu, pia uwezo wa kufasiri ndoto, kueleza mafumbo, na kutatua matatizo magumu. Mwite Danieli, naye atakuambia maana ya haya maandishi.”