Danieli 3:8-12
Danieli 3:8-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, baadhi ya Wakaldayo wakajitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Walimwambia mfalme Nebukadneza, “Uishi, ee mfalme! Wewe, ee mfalme, ulitoa amri kuwa kila mtu anaposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na kila aina ya muziki, ainame chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu. Na kwamba mtu yeyote asiyeinama chini na kuiabudu sanamu hiyo, atupwe ndani ya tanuri ya moto mkali. Sasa, kuna Wayahudi fulani uliowateua kushughulikia mambo ya utawala wa mkoa wa Babuloni, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego; watu hawa, ee mfalme, hawakuitii amri yako. Wanakataa kuitumikia miungu yako na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
Danieli 3:8-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi. Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadneza, Ee mfalme, uishi milele. Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zumari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu; na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuri liwakalo moto. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
Danieli 3:8-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi. Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadreza, Ee mfalme, uishi milele. Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu; na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya moto uwakao. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
Danieli 3:8-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele! Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari, na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima asujudu na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu, na kwamba yeyote ambaye hatasujudu na kuiabudu atatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli, yaani Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”