Danieli 3:13-18
Danieli 3:13-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo mfalme Nebukadneza, huku akiwaka hasira, akaamuru Shadraki, Meshaki na Abednego waletwe mbele yake. Nao wakawaleta mbele ya mfalme. Mfalme Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba wewe Shadraki, wewe Meshaki na wewe Abednego, hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi, mtakaposikia tena sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, santuri, zumari na sauti za ala nyingine za muziki, je, mko tayari kuinama chini na kuiabudu sanamu niliyotengeneza? Kama mkikataa, mtatupwa mara moja katika tanuri ya moto mkali. Je, ni mungu gani anayeweza kuwaokoa mikononi mwangu?” Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, sisi hatuhitaji kukujibu kuhusu jambo hilo. Ikiwa ndivyo, Mungu wetu ambaye tunamtumikia aweza kutuokoa katika tanuri ya moto mkali; tena atatuokoa mikononi mwako, ee mfalme. Lakini, hata kama haitafanyika hivyo, ujue wazi, ee mfalme, kwamba sisi hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyosimamisha.”
Danieli 3:13-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Nebukadneza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadneza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hamumtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zumari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuri liwakalo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi mikononi mwangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadneza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuri liwakalo moto; naye atatuokoa mkononi mwako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
Danieli 3:13-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
Danieli 3:13-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mfalme Nebukadneza, akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme, naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa hiyo hiyo ndani ya tanuru linalowaka moto. Naye ni mungu yupi ataweza kuwaokoa ninyi kutoka mkononi mwangu?” Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru linalowaka moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”