Danieli 12:1-3
Danieli 12:1-3 Biblia Habari Njema (BHN)
“ ‘Wakati huo, Mikaeli, malaika mkuu, aliye mlinzi wa watu wako, atatokea. Ndipo kutakuwa na wakati wa taabu sana kuliko nyakati nyingine zote tangu mataifa yalipoanza kuwako duniani. Lakini, wakati huo, kila mmoja wa watu wako ambaye jina lake limeandikwa katika kitabu cha uhai, ataokolewa. Wengi wa wale ambao wamekwisha kufa, watafufuka; wengine watapata uhai wa milele, na wengine watapata uhai na kudharauliwa milele. Wale wenye hekima watangaa kama anga angavu, na wale waliowaongoza wengine kutenda mema, watangaa kama nyota milele.
Danieli 12:1-3 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati huo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile. Tena, wengi wa hao wanaolala katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.
Danieli 12:1-3 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile. Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.
Danieli 12:1-3 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa. Wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwa aibu na kudharauliwa milele. Wale wenye hekima watangʼaa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watangʼaa kama nyota milele na milele.