Danieli 1:8-16
Danieli 1:8-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Danieli aliamua kutojitia unajisi kwa kula chakula bora cha mfalme na kunywa divai yake. Kwa hiyo, alimwomba towashi mkuu amruhusu asile vitu hivyo na kujitia unajisi. Basi, Mungu akamjalia Danieli kupendelewa na kuhurumiwa na Ashpenazi, towashi mkuu. Lakini, towashi mkuu akamwambia Danieli, “Nina hofu kwamba bwana wangu mfalme ambaye ametoa maagizo kuhusu chakula na vinywaji unavyopaswa kutumia, ataona kuwa afya yako si nzuri kama ya wenzako wa rika lako. Hivyo maisha yangu yatakuwa hatarini.” Hapo Danieli akamwendea mtumishi aliyewekwa na towashi mkuu kumlinda yeye na wenzake kina Hanania, Mishaeli na Azaria, akamwambia, “Tafadhali utujaribu, sisi watumishi wako kwa muda wa siku kumi kwa kutupa mboga za majani na maji. Kisha, tulinganishe sisi na hao vijana wengine wanaokula chakula cha mfalme, halafu utoe uamuzi wako kulingana na jinsi utakavyoona.” Mlinzi akakubaliana nao, akawajaribu kwa muda wa siku kumi. Baada ya siku hizo kumi, aliwaangalia akaona kuwa wale vijana waliokula mboga za majani walionekana wenye afya na nguvu kuliko wale wengine wote waliolishwa chakula cha kifalme. Basi, yule mlinzi akawaacha waendelee kula mboga za majani badala ya chakula cha fahari na divai.
Danieli 1:8-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi. Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi. Mkuu wa matowashi akamwambia Danieli, Mimi namwogopa bwana wangu, mfalme, aliyewaagizia ninyi chakula chenu na kinywaji chenu; kwa nini azione nyuso zenu kuwa hazipendezi kama nyuso za vijana wa rika lenu? Basi kwa kufanya hivyo mtahatarisha kichwa changu mbele ya mfalme. Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria, Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mboga za majani tule, na maji tunywe. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona. Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi. Hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi, na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme. Basi yule msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula, na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama tu.
Danieli 1:8-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi. Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi. Mkuu wa matowashi akamwambia Danieli, Mimi namwogopa bwana wangu, mfalme, aliyewaagizia ninyi chakula chenu na kinywaji chenu; kwa nini azione nyuso zenu kuwa hazipendezi kama nyuso za vijana hirimu zenu? Basi kwa kufanya hivyo mtahatirisha kichwa changu mbele ya mfalme. Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria, Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama tule, na maji tunywe. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona. Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi. Hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi, na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme. Basi yule msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula, na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama tu.
Danieli 1:8-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajinajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii. Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonesha upendeleo na huruma kwa Danieli. Lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu zikiwa mbaya kuliko za vijana wengine wa rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.” Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, “Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majani tule, na maji ya kunywa. Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.” Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi. Mwisho wa zile siku kumi, walionekana kuwa na afya na kunawiri kuliko yeyote kati ya vijana waliokula chakula cha mfalme. Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa, akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.