Danieli 1:11-14
Danieli 1:11-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo Danieli akamwendea mtumishi aliyewekwa na towashi mkuu kumlinda yeye na wenzake kina Hanania, Mishaeli na Azaria, akamwambia, “Tafadhali utujaribu, sisi watumishi wako kwa muda wa siku kumi kwa kutupa mboga za majani na maji. Kisha, tulinganishe sisi na hao vijana wengine wanaokula chakula cha mfalme, halafu utoe uamuzi wako kulingana na jinsi utakavyoona.” Mlinzi akakubaliana nao, akawajaribu kwa muda wa siku kumi.
Danieli 1:11-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria, Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mboga za majani tule, na maji tunywe. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona. Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi.
Danieli 1:11-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria, Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama tule, na maji tunywe. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona. Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi.
Danieli 1:11-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, “Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majani tule, na maji ya kunywa. Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.” Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi.