Wakolosai 4:7-12
Wakolosai 4:7-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote. Ndiyo maana ninamtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu. Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa. Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni). Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu. Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimuni. Daima anawaombeeni nyinyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu.
Wakolosai 4:7-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mwenzi wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote; ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu; pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa petu. Aristarko, aliyefungwa pamoja nami, awasalimu; pamoja na Marko, binamu yake Barnaba, ambaye mmepokea maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni. Na Yesu aitwaye Yusto awasalimu. Hao tu ndio watu wa tohara miongoni mwa wale watendao kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu; nao wamekuwa msaada kwangu. Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili msimame mkiwa wakamilifu na kuthibitika kabisa katika mapenzi yote ya Mungu.
Wakolosai 4:7-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mjoli wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote; ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu; pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa petu. Aristarko, aliyefungwa pamoja nami, awasalimu; na Marko, mjomba wake Barnaba, ambaye mmepokea maagizo kwa habari yake; akifika kwenu mkaribisheni. Na Yesu aitwaye Yusto; hao ni watu wa tohara. Tena hao peke yao ni watendaji wa kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu; nao walikuwa faraja kwangu. Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu.
Wakolosai 4:7-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtendakazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana. Nimemtuma kwenu kwa lengo maalum la kuwafahamisha hali yetu, na pia awatie moyo. Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu. Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni.) Yesu aitwaye Yusto pia anawasalimu. Hawa peke yao ndio Wayahudi miongoni mwa watendakazi wenzangu kwa ajili ya ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu. Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu, mkiwa wakamilifu na thabiti.