Wakolosai 4:2-9
Wakolosai 4:2-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu. Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni. Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo. Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri wakati mlio nao. Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na yaliyokolezwa kwa chumvi na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja. Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote. Ndiyo maana ninamtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu. Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa.
Wakolosai 4:2-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba mkiwa na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena. Nendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolezwa chumvi, ili mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu. Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mwenzi wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote; ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu; pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa petu.
Wakolosai 4:2-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena. Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu. Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mjoli wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote; ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu; pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa petu.
Wakolosai 4:2-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru. Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena neno lake, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa. Ombeni ili nipate kuitangaza hiyo siri kwa udhahiri kama inipasavyo. Nendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu. Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtendakazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana. Nimemtuma kwenu kwa lengo maalum la kuwafahamisha hali yetu, na pia awatie moyo. Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu.