Wakolosai 3:1-7
Wakolosai 3:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, ameketi upande wa kulia wa Mungu. Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani. Maana nyinyi mmekufa na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Uhai wenu halisi ni Kristo, na wakati atakapotokea ndipo nanyi pia mtakapotokea pamoja naye katika utukufu. Basi, ueni chochote kilicho ndani yenu ambacho ni cha kidunia: Uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu). Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi. Wakati mmoja nyinyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo.
Wakolosai 3:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi katika mkono wa kulia wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu. Basi, viueni viungo vyenu vilivyo vya kidunia, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu. Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo.
Wakolosai 3:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu. Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu. Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo.
Wakolosai 3:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo, aliye uzima wenu, atakapofunuliwa, ndipo nanyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu. Basi, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambao ni ibada ya sanamu. Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo.