Wakolosai 2:6-12
Wakolosai 2:6-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Maadamu nyinyi mmemkubali Kristo Yesu aliye Bwana, basi, ishini katika muungano naye. Muwe na mizizi ndani yake, mjijenge juu yake na kuwa imara katika imani kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele. Angalieni, basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe! Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu, nanyi mmepewa uhai kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote. Katika kuungana na Kristo nyinyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi. Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo mlifufuliwa pia pamoja naye kwa kuamini katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka kwa wafu.
Wakolosai 2:6-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, ishini vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo. Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.
Wakolosai 2:6-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo. Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.
Wakolosai 2:6-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, mkijikita na kujengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani. Chungeni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu, yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Kristo. Maana utimilifu wote wa Mungu unakaa ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, aliye mkuu juu ya kila nguvu na kila mamlaka. Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo, mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kupitia kwa imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.