Wakolosai 2:1-15
Wakolosai 2:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Napenda mjue jinsi ninavyofanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, kwa ajili ya watu wa Laodikea na kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona kwa macho. Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe. Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu. Basi, nawaambieni, msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa maneno ya uongo hata kama ni ya kuvutia sana. Maana, ingawa mimi niko mbali nanyi kwa mwili, lakini niko pamoja nanyi kwa roho, na ninafurahi kuona uthabiti kamili mnaosimama nao pamoja katika imani yenu kwa Kristo. Maadamu nyinyi mmemkubali Kristo Yesu aliye Bwana, basi, ishini katika muungano naye. Muwe na mizizi ndani yake, mjijenge juu yake na kuwa imara katika imani kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele. Angalieni, basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe! Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu, nanyi mmepewa uhai kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote. Katika kuungana na Kristo nyinyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi. Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo mlifufuliwa pia pamoja naye kwa kuamini katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka kwa wafu. Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu nyinyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa nyinyi uhai pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote; alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani. Huko Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake.
Wakolosai 2:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana nataka ninyi mjue jinsi ilivyo kuu juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na wale wasioniona uso wangu katika mwili; ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika. Nasema neno hili, mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kuwashawishi. Maana nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho, nikifurahi na kuuona utaratibu wenu na uthabiti wa imani yenu katika Kristo. Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, ishini vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo. Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu. Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutotahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuziaibisha hadharani, akiziongoza kwa ushindi wake wa shangwe.
Wakolosai 2:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana nataka ninyi mjue jinsi ilivyo kuu juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na wale wasioniona uso wangu katika mwili; ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika. Nasema neno hili, mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kuwashawishi. Maana nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho, nikifurahi na kuuona utaratibu wenu na uthabiti wa imani yenu katika Kristo. Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo. Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu. Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.
Wakolosai 2:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walio Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi. Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani Kristo, ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa. Nawaambia mambo haya ili mtu yeyote asiwadanganye kwa maneno matamu. Kwa kuwa ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi uthabiti wa imani yenu katika Kristo ulivyo. Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, mkijikita na kujengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani. Chungeni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu, yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Kristo. Maana utimilifu wote wa Mungu unakaa ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, aliye mkuu juu ya kila nguvu na kila mamlaka. Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo, mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kupitia kwa imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu. Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, baada ya kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akaigongelea kwenye msalaba wake. Baada ya Mungu kuzivua enzi na mamlaka, aliziaibisha hadharani, akishangilia katika ushindi wa msalaba.