Amosi 9:7-15
Amosi 9:7-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kwangu mimi, nyinyi Waisraeli, hamna tofauti yoyote na watu wa Kushi! Niliwatoa Wafilisti kutoka Krete, na Waashuru kutoka Kiri, kama nilivyowatoa nyinyi kutoka Misri. Mimi, Bwana Mwenyezi-Mungu nautazama ufalme wenye dhambi, na nitauangamiza kabisa kutoka duniani. Lakini sitawaangamiza wazawa wote wa Yakobo. “Tazama, nitatoa amri, na kuwapepeta Waisraeli kati ya mataifa kama mtu achekechavyo nafaka niwakamate wote wasiofaa. Wenye dhambi miongoni mwa watu wangu, watafia vitani kwa upanga; hao ndio wasemao: ‘Maafa hayatatukumba wala kutupata!’ “Siku yaja nitakapoisimika nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitazitengeneza kuta zake, na kusimika upya magofu yake. Nitaijenga upya kama ilivyokuwa hapo zamani. Nao Waisraeli watamiliki mabaki ya Edomu na mataifa yote yaliyokuwa yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, na nitafanya hivyo. “Wakati waja kwa hakika, ambapo mara baada ya kulima mavuno yatakuwa tayari kuvunwa; mara baada ya kupanda mizabibu utafuata wakati wa kuvuna zabibu. Milima itabubujika divai mpya, navyo vilima vitatiririka divai. Nitarekebisha hali ya watu wangu Waisraeli. Watajenga miji yao iliyoharibiwa na kuishi humo; watapanda mizabibu na kunywa divai yake; watalima mashamba na kula mazao yake. Nitawasimika katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena kutoka katika nchi niliyowapa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Amosi 9:7-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Je! Ninyi si kama wana wa Wakushi kwangu mimi, enyi wana wa Israeli, asema BWANA? Je! Mimi sikuwapandisha Israeli toka nchi ya Misri, na Wafilisti toka Kaftori, na Washami toka Kiri? Angalieni, macho ya Bwana MUNGU yanauangalia ufalme wenye dhambi, nami nitauangamiza utoke juu ya uso wa dunia; lakini sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo, asema BWANA. Kwa maana, angalieni, nitatoa amri, nami nitaipepeta nyumba ya Israeli katika mataifa yote, kama vile ngano ipepetwavyo katika ungo lakini hata chembe moja iliyo ndogo haitaanguka chini. Wenye dhambi wote katika watu wangu watakufa kwa upanga, hao wasemao, Mabaya hayatatupata nyuma wala mbele. Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema BWANA, afanyaye hayo. Angalieni, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo huyo alimaye atamfikia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka. Nami nitawarejesha tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watatengeneza bustani, na kula matunda yake. Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema BWANA, Mungu wako.
Amosi 9:7-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Je! Ninyi si kama wana wa Wakushi kwangu mimi, enyi wana wa Israeli, asema BWANA? Je! Mimi sikuwapandisha Israeli toka nchi ya Misri, na Wafilisti toka Kaftori, na Washami toka Kiri? Angalieni, macho ya Bwana MUNGU yanauangalia ufalme wenye dhambi, nami nitauangamiza utoke juu ya uso wa dunia; lakini sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo, asema BWANA. Kwa maana, angalieni, nitatoa amri, nami nitaipepeta nyumba ya Israeli katika mataifa yote, kama vile ngano ipepetwavyo katika ungo lakini hata chembe moja iliyo ndogo haitaanguka chini. Wenye dhambi wote katika watu wangu watakufa kwa upanga, hao wasemao, Mabaya hayatatupata nyuma wala mbele. Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale; wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema BWANA, afanyaye hayo. Angalieni, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka. Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda yake. Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang’olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema BWANA, Mungu wako.
Amosi 9:7-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Je, Waisraeli, ninyi si sawa kwangu kama Wakushi?” asema BWANA. “Je, sikuleta Israeli kutoka Misri, Wafilisti kutoka Kaftori, na Washamu kutoka Kiri? “Hakika macho ya BWANA Mwenyezi yako juu ya ufalme wenye dhambi. Nami nitauangamiza kutoka uso wa dunia: hata hivyo sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo,” asema BWANA. “Kwa kuwa nitatoa amri, na nitaipepeta nyumba ya Israeli miongoni mwa mataifa yote, kama vile nafaka ipepetwavyo katika ungo, na hakuna hata punje moja itakayoanguka chini. Watenda dhambi wote miongoni mwa watu wangu watauawa kwa upanga, wale wote wasemao, ‘Maafa hayatatupata wala kutukuta.’ “Katika siku ile “Nitalisimamisha hema la Daudi lililoanguka. Nitakarabati mahali palipobomoka na kujenga upya magofu yake, na kuijenga kama ilivyokuwa awali, ili wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yale yanayobeba Jina langu,” asema BWANA ambaye atafanya mambo haya. “Siku zinakuja,” asema BWANA, “wakati mvunaji atatanguliwa na mkulima, naye mpanzi atatanguliwa na yeye akamuaye zabibu. Divai mpya itadondoka kutoka milimani, na kutiririka kutoka vilima vyote. Nitawarejesha tena watu wangu Israeli waliohamishwa; wataijenga tena miji iliyoachwa magofu, nao wataishi ndani yake. Watapanda mizabibu na kunywa divai yake; watalima bustani na kula matunda yake. Nitaipanda Israeli katika nchi yao wenyewe, hawatangʼolewa tena kutoka nchi niliyowapa,” asema BWANA Mungu wenu.