Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Amosi 8:1-14

Amosi 8:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Niliona kikapu kilichojaa matunda ya kiangazi. Naye Mwenyezi-Mungu akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nami nikamjibu, “Naona kikapu cha matunda ya kiangazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Mwisho umewafikia watu wangu wa Israeli. Sitavumilia tena maovu yao. Siku hiyo, nyimbo za ikulu zitakuwa maombolezo. Kutakuwa na maiti nyingi, nazo zitatupwa nje kimyakimya.” Sikilizeni enyi mnaowakandamiza wanyonge na kuwaletea maangamizi fukara wa nchi. Mnajisemea mioyoni mwenu: “Sikukuu ya mwezi mwandamo itakwisha lini ili tuanze tena kuuza nafaka yetu? Siku ya Sabato itakwisha lini ili tupate kuuza ngano yetu? Tutatumia vipimo hafifu vya wastani na uzito, tutadanganya watu kwa mizani isizo sawa, hata kuuza ngano hafifu kwa bei kubwa. Tutaweza kununua watu fukara kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya kandambili.” Mwenyezi-Mungu, fahari ya Yakobo, ameapa: “Hakika, sitayasahau matendo yao maovu. Kwa hiyo, dunia itatetemeka na kila mtu nchini ataomboleza. Nchi yote itayumbayumba; itapanda na kushuka, kama yanavyojaa na kupwa maji ya mto Nili!” Bwana Mwenyezi-Mungu asema, “Siku hiyo nitalifanya jua litue adhuhuri, na kuijaza nchi giza mchana. Sherehe zenu nitazigeuza kuwa kilio, na nyimbo zenu za furaha kuwa maombolezo. Nitawafanya nyote mvae magunia kwa huzuni na kunyoa vipara vichwa vyenu, kama kuomboleza kifo cha mtoto wa pekee; na siku ya mwisho itakuwa ya uchungu mkubwa.” Bwana Mwenyezi-Mungu asema, “Siku zaja ambapo nitaleta njaa nchini. Lakini sio njaa na kiu ya chakula na maji, bali njaa ya kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu. Watu watatangatanga kutoka bahari hata bahari, kutoka upande wa kaskazini mpaka mashariki. Watakimbia huko na huko wakitafuta neno la Mwenyezi-Mungu, lakini hawatalipata. “Siku hiyo, hata vijana wenye afya, wa kiume kwa wa kike, watazimia kwa kiu. Wale wanaoapa kwa mungu wa uongo wa Samaria, na kusema: ‘Kwa nafsi ya mungu wako ee Dani’; na, ‘Kwa nafsi ya mungu wa Beer-sheba’, wote wataanguka na hawatainuka tena kamwe.”

Shirikisha
Soma Amosi 8

Amosi 8:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Haya ndiyo aliyonionesha Bwana MUNGU; tazama, kikapu cha matunda ya wakati wa joto. Akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona kikapu cha matunda ya wakati wa joto. Ndipo BWANA akaniambia, Mwisho wao watu wangu Israeli umewajia; sitawapita tena kamwe. Tena nyimbo za hekaluni zitakuwa vilio siku ile, asema Bwana MUNGU; mizoga itakuwa mingi; kila mahali wataitupa, wakinyamaza kimya. Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandaa ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu; tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano. BWANA ameapa kwa fahari ya Yakobo, Hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo. Kwa ajili ya hayo, je! Haitatetemeka nchi, na kuomboleza kila mtu akaaye ndani yake? Naam, itainuka yote pia kama huo Mto; nayo itataabika na kupwa tena kama Mto wa Misri. Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru ya mchana. Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upara katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu. Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA. Nao watatangatanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huku na huko, kulitafuta neno la BWANA, wasilione. Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu. Na hao waapao kwa dhambi ya Samaria, na kusema, Kama aishivyo Mungu wako, Ee Dani, na, Kama iishivyo njia ya Beer-sheba, hao nao wataanguka, wasiinuke tena.

Shirikisha
Soma Amosi 8

Amosi 8:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, kikapu cha matunda ya wakati wa hari. Akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona kikapu cha matunda ya wakati wa hari. Ndipo BWANA akaniambia, Mwisho wao umewajilia watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe. Tena nyimbo za hekaluni zitakuwa vilio siku ile, asema Bwana MUNGU; mizoga itakuwa mingi; kila mahali wataitupa, wakinyamaza kimya. Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi, mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu; tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano. BWANA ameapa kwa fahari ya Yakobo, Hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo. Kwa ajili ya hayo, je! Haitatetemeka nchi, na kuomboleza kila mtu akaaye ndani yake? Naam, itainuka yote pia kama huo Mto; nayo itataabika na kupwa tena kama Mto wa Misri. Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru ya mchana. Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu. Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya BWANA. Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la BWANA, wasilione. Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu. Na hao waapao kwa dhambi ya Samaria, na kusema, Kama aishivyo Mungu wako, Ee Dani, na, Kama iishivyo njia ya Beer-sheba, hao nao wataanguka, wasiinuke tena.

Shirikisha
Soma Amosi 8

Amosi 8:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hili ndilo alilonionesha BWANA Mwenyezi katika maono: kikapu cha matunda yaliyoiva. Akaniuliza, “Amosi, unaona nini?” Nikajibu, “Kikapu chenye matunda yaliyoiva.” Ndipo BWANA akaniambia, “Wakati umewadia kwa watu wangu Israeli; sitawahurumia zaidi.” BWANA Mwenyezi asema, “Katika siku ile, nyimbo katika Hekalu zitageuka kuwa maombolezo. Miili mingi, mingi sana: itatupwa kila mahali! Kimya!” Lisikieni hili, ninyi ambao mnawagandamiza wahitaji, na kuwaonea maskini wa nchi, mkisema, “Ni lini Mwezi Mwandamo utakapopita ili tupate kuuza nafaka, na Sabato itakwisha lini ili tuweze kuuza ngano?” Mkipunguza vipimo, na kuongeza bei, na kudanganya kwa mizani zisizo sawa, mkiwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu, na mkiuza hata takataka za ngano pamoja na ngano. BWANA ameapa kwake mwenyewe, aliye Fahari ya Yakobo: “Kamwe sitasahau chochote ambacho wamefanya. “Je, nchi haitatetemeka kwa ajili ya hili, nao wote wanaoishi ndani yake hawataomboleza? Nchi yote itainuka kama Mto Naili; itapanda na kushuka kama mto wa Misri. “Katika siku ile,” asema BWANA Mwenyezi, “Nitalifanya jua litue alasiri na kuifanya dunia iwe giza wakati wa mchana mwangavu. Nitageuza sikukuu zenu za kidini kuwa maombolezo, na kuimba kwenu kote kuwe kilio. Nitawafanya ninyi nyote mvae magunia na kunyoa nywele zenu. Nitaufanya wakati ule uwe kama wa kuombolezea mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu. “Siku zinakuja,” asema BWANA Mwenyezi, “wakati nitakapotuma njaa katika nchi yote: si njaa ya chakula wala kiu ya maji, lakini njaa ya kusikia maneno ya BWANA. Wanaume watayumbayumba kutoka bahari hadi bahari na kutangatanga kutoka kaskazini mpaka mashariki, wakitafuta neno la BWANA, lakini hawatalipata. “Katika siku ile “wasichana wazuri na wavulana wenye nguvu watazimia kwa sababu ya kiu. Wale waapao kwa aibu ya Samaria, au kusema, ‘Hakika kama miungu yenu iishivyo, ee Dani,’ au ‘Hakika kama mungu wa Beer-Sheba aishivyo’: wataanguka, wala hawatasimama tena.”

Shirikisha
Soma Amosi 8