Amosi 7:1-17
Amosi 7:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono: Nilimwona Mungu anaumba nzige kundi zima, mara baada ya watu kumaliza kukata nyasi kwa ajili ya wanyama wa mfalme. Wakati huo, nyasi zilikuwa ndio zinaanza kuchipua tena. Niliwaona nzige hao wakila na kumaliza kila jani katika nchi. Ndipo nikasema: “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi utuhurumie! Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi? Wao ni wadogo mno!” Basi, Bwana Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake, akasema, “Haitakuwa hivyo!” Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Nilimwona Bwana Mwenyezi-Mungu akiuita moto wa hukumu ya kuwaadhibu watu. Moto huo uliunguza vilindi vikuu vya bahari, ukaanza kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema: “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi uache kuadhibu! Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi? Wao ni wadogo mno!” Basi, Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake, akasema: “Hili pia halitatukia.” Mwenyezi-Mungu alinijalia tena maono mengine: Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama karibu na ukuta, ameshika mkononi mwake uzi wenye timazi. Naye akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nikamjibu, “Naona timazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akasema: “Tazama! Naweka timazi kati ya watu wangu Waisraeli. Sitavumilia tena maovu yao. Huko vilimani ambako wazawa wa Isaka hutambikia, kutafanywa kuwa uharibifu mtupu na maskani ya Waisraeli yatakuwa magofu. Nitaushambulia kwa vita ukoo wa mfalme Yeroboamu.” Basi, Amazia kuhani wa mji wa Betheli, akampelekea mfalme Yeroboamu wa Israeli habari hizi: “Amosi analeta fitina juu yako katika ufalme wa Israeli. Hotuba zake ni hatari kwa nchi hii. Anachosema ni hiki: ‘Yeroboamu atakufa kwa upanga nao Waisraeli watapelekwa uhamishoni, mbali kabisa na nchi yao.’” Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Sasa tumekuchoka, ewe nabii! Nenda zako! Rudi katika nchi ya Yuda, ukatoe unabii huko upate na ujira wako hukohuko. Usitoe tena unabii hapa mjini Betheli, kwa kuwa hapa ni maskani ya ibada ya mfalme; ni hekalu la utawala huu.” Amosi akamjibu Amazia, “Mimi si nabii wa kuajiriwa, wala si mmoja wa kikundi cha manabii. Mimi ni mchungaji na mtunza mikuyu. Mwenyezi-Mungu alinitoa katika kazi yangu hiyo ya uchungaji, akaniamuru nije kuwaambia unabii watu wake wa Israeli. Nawe basi, ewe Amazia, sikiliza neno la Mwenyezi-Mungu: Wewe waniambia nisitoe unabii dhidi ya Israeli, wala nisihubiri dhidi ya wazawa wa Isaka. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Mkeo atakuwa malaya mjini, na wanao wa kiume na kike watauawa vitani. Ardhi yako itagawanywa na kupewa wengine, nawe binafsi utafia katika nchi najisi, nao Waisraeli hakika watapelekwa uhamishoni, mbali kabisa na nchi yao.’”
Amosi 7:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya ndiyo aliyonionesha Bwana MUNGU; tazama, aliumba nzige mwanzo wa kuchipuka kwake mimea wakati wa vuli; na tazama, ilikuwa mimea ya wakati wa vuli baada ya mavuno ya mfalme. Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, samehe, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili. Jambo hili halitakuwa, asema BWANA. Haya ndiyo aliyonionesha Bwana MUNGU; tazama, Bwana MUNGU aliita ili kushindana kwa moto; nao ukaviteketeza vilindi vikuu, ukataka kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, acha, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili pia. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana MUNGU. Haya ndiyo aliyonionesha; na tazama, Bwana alisimama karibu na ukuta uliojengwa kwa timazi, mwenye timazi mkononi mwake. BWANA akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona timazi. Ndipo Bwana akasema, Tazama, nitaweka timazi kati ya watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe; na mahali palipoinuka pa Isaka patakuwa ukiwa, na mahali patakatifu pa Israeli pataharibika; nami nitaondoka nishindane na nyumba ya Yeroboamu kwa upanga. Ndipo Amazia, kuhani wa Betheli, akapeleka habari kwa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akisema, Amosi amefanya fitina juu yako kati ya nyumba ya Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote. Kwa maana Amosi asema hivi, Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atapelekwa uhamishoni, mbali na nchi yake. Tena Amazia akamwambia Amosi, Ewe mwonaji, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nilikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye BWANA akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Nenda uwatabirie watu wangu Israeli. Basi, sasa lisikie neno la BWANA; Wewe unasema, Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya Isaka; kwa hiyo, BWANA asema hivi, Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba; na wewe mwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli atapelekwa uhamishoni mbali na nchi yake.
Amosi 7:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, aliumba nzige mwanzo wa kuchipuka kwake mimea wakati wa vuli; na tazama, ilikuwa mimea ya wakati wa vuli baada ya mavuno ya mfalme. Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, samehe, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili. Jambo hili halitakuwa, asema BWANA. Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, Bwana MUNGU aliita ili kushindana kwa moto; nao ukavila vilindi vikuu, ukataka kuiteketeza nchi kavu. Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, acha, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili pia. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana MUNGU. Haya ndiyo aliyonionyesha; na tazama, Bwana alisimama karibu na ukuta uliojengwa kwa timazi, mwenye timazi mkononi mwake. BWANA akaniambia, Amosi, unaona nini? Nikasema, Naona timazi. Ndipo Bwana akasema, Tazama, nitaweka timazi kati ya watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe; na mahali palipoinuka pa Isaka patakuwa ukiwa, na mahali patakatifu pa Israeli pataharibika; nami nitaondoka nishindane na nyumba ya Yeroboamu kwa upanga. Ndipo Amazia, kuhani wa Betheli, akapeleka habari kwa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akisema, Amosi amefanya fitina juu yako kati ya nyumba ya Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote. Kwa maana Amosi asema hivi, Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali, hali ya kufungwa, atoke katika nchi yake. Tena Amazia akamwambia Amosi, Ewe mwonaji, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye BWANA akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli. Basi, sasa lisikie neno la BWANA; Wewe unasema, Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya Isaka; kwa hiyo, BWANA asema hivi, Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba; na wewe mwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali hali ya kufungwa kutoka nchi yake.
Amosi 7:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hili ndilo alilonionesha BWANA Mwenyezi katika maono: Alikuwa anaandaa makundi ya nzige baada ya kuvunwa fungu la mfalme na wakati ule tu mimea ya pili ilipokuwa ikichipua. Wakati nzige walikuwa wamekula mimea yote ya nchi, nililia kwa sauti kuu, “BWANA Mwenyezi, samehe! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!” Kwa hiyo BWANA akaghairi. Kisha BWANA akasema, “Hili halitatokea.” Hili ndilo BWANA Mwenyezi alilonionesha katika maono: BWANA Mwenyezi alikuwa akiita hukumu ya moto; nao ulikausha vilindi vikuu, ukateketeza nchi. Ndipo nikalia, “BWANA Mwenyezi, nakusihi, zuia! Je, Yakobo atawezaje kuendelea kuishi? Yeye ni mdogo sana!” Kwa hiyo BWANA akaghairi. BWANA Mwenyezi akasema, “Hili nalo halitatokea.” Hili ndilo alilonionesha katika maono: Bwana alikuwa amesimama karibu na ukuta ambao ulikuwa umejengwa kwa timazi, akiwa na uzi wa timazi mkononi mwake. Naye BWANA akaniuliza, “Je, Amosi unaona nini?” Nikamjibu, “Uzi wa timazi.” Kisha Bwana akasema, “Tazama, ninaweka uzi wa timazi miongoni mwa watu wangu Israeli; sitawahurumia tena. “Mahali pa Isaka pa juu pa kuabudia pataangamizwa, na mahali patakatifu pa Israeli pa kuabudia pataharibiwa; kwa upanga wangu nitainuka dhidi ya nyumba ya Yeroboamu.” Kisha Amazia kuhani wa Betheli akatuma ujumbe kwa Yeroboamu mfalme wa Israeli, akisema: “Amosi analeta fitina juu yako katikati ya Israeli. Nchi haiwezi kuvumilia maneno yake yote. Kwa kuwa hili ndilo Amosi analosema: “ ‘Yeroboamu atakufa kwa upanga, na kwa hakika Israeli wataenda uhamishoni, mbali na nchi yao.’ ” Kisha Amazia akamwambia Amosi, “Nenda zako, ewe mwonaji! Urudi katika nchi ya Yuda. Ujipatie riziki yako huko na kutoa unabii wako. Usiendelee kutoa unabii katika Betheli, kwa sababu hapa ni mahali pa mfalme pa kuabudia na Hekalu la ufalme huu.” Amosi akamjibu Amazia, “Mimi sikuwa nabii wala mwana wa nabii, lakini nilikuwa mchungaji wa kondoo na mtunza mikuyu. Lakini BWANA akanitoa kutoka kuchunga kondoo na kuniambia, ‘Nenda, ukawatabirie watu wangu Israeli.’ Sasa basi, sikieni neno la BWANA. Ninyi mnasema, “ ‘Usitabiri dhidi ya Israeli, na uache kuhubiri dhidi ya nyumba ya Isaka.’ “Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA: “ ‘Mke wako atakuwa kahaba mjini, nao wana wako wa kiume na wa kike watauawa kwa upanga. Shamba lako litapimwa na kugawanywa, na wewe mwenyewe utafia katika nchi ya kipagani. Nayo Israeli kwa hakika itaenda uhamishoni, mbali na nchi yao.’ ”