Amosi 6:1-7
Amosi 6:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wenu nyinyi mnaostarehe huko Siyoni, nanyi mnaojiona salama mlimani Samaria! Nyinyi mwaonekana kuwa viongozi wa taifa maarufu ambao Waisraeli wote huwategemea. Haya! Nendeni Kalne mkaangalie kila mahali, tokeni huko mwende hadi mji ule mkubwa wa Hamathi, kisha teremkeni hadi Gathi kwa Wafilisti. Je, falme zao si bora kuliko zenu na eneo lao si bora kuliko lenu?” Nyinyi mnajaribu kuifukuza siku mbaya. Lakini mnauleta karibu utawala dhalimu. Ole wenu mnaolala juu ya vitanda vya pembe za ndovu na kujinyosha juu ya masofa, mkila nyama za wanakondoo na ndama! Nyinyi mnapenda kuimba ovyo na sauti ya vinubi na kubuni ala mpya za muziki mkimwiga mfalme Daudi. Mnakunywa divai kwa mabakuli, na kujipaka marashi mazuri mno. Lakini hamhuzuniki hata kidogo juu ya kuangamia kwa wazawa wa Yosefu. Kwa hiyo mtakuwa wa kwanza kwenda uhamishoni, na karamu za wenye kustarehe zitatoweka.
Amosi 6:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea. Piteni hadi Kalne, mkaone; tena tokea huko nendeni hadi Hamathi iliyo kuu; kisha shukeni hadi Gathi ya Wafilisti; je! Ninyi ni bora kuliko falme hizi? Au eneo lao ni kubwa kuliko eneo lenu? Ninyi mnaoiweka mbali siku hiyo mbaya, na kulileta karibu kao la udhalimu; ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya makochi yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini; ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi; ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu. Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za shangwe za hao waliojinyosha zitakoma.
Amosi 6:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea. Piteni hata Kalne, mkaone; tena tokea huko enendeni hata Hamathi iliyo kuu; kisha shukeni hata Gathi ya Wafilisti; je! Ninyi ni bora kuliko falme hizi? Au mpaka wao ni mkubwa kuliko mpaka wenu? Ninyi mnaoiweka mbali siku hiyo mbaya, na kulileta karibu kao la udhalimu; ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya masemadari yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini; ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi; ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu. Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za machezo za hao waliojinyosha zitakoma.
Amosi 6:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni, na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria, ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine, ambao watu wa Israeli wanawategemea! Nendeni Kalne mkaone kutoka huko; mwende hadi Hamathi iliyo kuu, kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti. Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili? Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu? Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya na kuleta karibu utawala wa kuogofya. Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu, na kujinyoosha juu ya viti vya fahari. Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri na ndama walionenepeshwa. Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi, huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali. Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa, na mnajipaka mafuta mazuri, lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yusufu. Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni; karamu zenu na kustarehe kutakoma.