Amosi 4:6-13
Amosi 4:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mimi niliwanyima chochote cha kutafuna, nikasababisha ukosefu wa chakula popote. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Tena niliwanyima mvua miezi mitatu tu kabla ya mavuno. Niliunyeshea mvua mji mmoja, na mji mwingine nikaunyima. Shamba moja lilipata mvua, na lingine halikupata, likakauka. Watu wa miji miwili, mitatu wakakimbilia mji mwingine, wapate maji, lakini hayakuwatosha. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Niliwapiga pigo la ukame na ukungu; nikakausha bustani na mashamba yenu ya mizabibu; nzige wakala mitini na mizeituni yenu. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Niliwaleteeni ugonjwa wa tauni kama ule nilioupelekea Misri. Niliwaua vijana wenu vitani, nikawachukua farasi wenu wa vita. Maiti zilijaa katika kambi zenu, uvundo wake ukajaa katika pua zenu. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Niliwaangusha baadhi yenu kwa maangamizi kama nilivyoangamiza Sodoma na Gomora. Wale walionusurika miongoni mwenu, walikuwa kama kijiti kilichookolewa motoni. Hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Kwa hiyo, enyi Waisraeli, nitawaadhibu. Na kwa kuwa nitafanya jambo hilo, kaeni tayari kuikabili hukumu yangu!” Mungu ndiye aliyeifanya milima, na kuumba upepo; ndiye amjulishaye mwanadamu mawazo yake; ndiye ageuzaye mchana kuwa usiku, na kukanyaga vilele vya dunia. Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lake!
Amosi 4:6-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mimi nami nimewapa usafi wa meno katika miji yenu yote, na kutindikiwa na mkate mahali penu pote; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Tena nimeizuia mvua msiipate, ilipobaki miezi mitatu kabla ya mavuno; nami nimenyesha mvua juu ya mji mmoja, nikaizuia mvua isinyeshe juu ya mji mwingine; sehemu moja ilipata mvua, na sehemu isiyopata mvua ilikauka. Basi kutoka miji miwili mitatu walitangatanga kuendea mji mwingine wapate kunywa maji, wasipate ya kuwatosha; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Nami nimewapiga kwa ukame na kuvu; wingi wa bustani zenu na mashamba yenu ya mizabibu, na mitini yenu na mizeituni yenu imeliwa na tunutu; Lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Nimewaletea tauni, kama tauni ya Misri; vijana wenu nimewaua kwa upanga, na farasi wenu nimewachukulia mbali; nami nimeupandisha uvundo wa kambi zenu na kuuingiza katika mianzi ya pua zenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli, na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli. Kwa maana, angalia, yeye aifanyaye milima, na kuumba upepo, na kumwambia mwanadamu mawazo yake, afanyaye asubuhi kuwa giza, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka; BWANA, Mungu wa majeshi, ndilo jina lake.
Amosi 4:6-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mimi nami nimewapa usafi wa meno katika miji yenu yote, na kutindikiwa na mkate mahali penu pote; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Tena nimeizuia mvua msiipate, ilipobaki miezi mitatu kabla ya mavuno; nami nimenyesha mvua juu ya mji mmoja, nikaizuia mvua isinyeshe juu ya mji mwingine; sehemu moja ilipata mvua, na sehemu isiyopata mvua ilikatika. Basi kutoka miji miwili mitatu walitanga-tanga kuendea mji mwingine wapate kunywa maji, wasipate ya kuwatosha; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Nami nimewapiga kwa ukavu na koga; wingi wa bustani zenu na mashamba yenu ya mizabibu, na mitini yenu na mizeituni yenu imeliwa na tunutu; Lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Nimewapelekea tauni, kama tauni ya Misri; vijana wenu nimewaua kwa upanga, na farasi wenu nimewachukulia mbali; nami nimeupandisha uvundo wa matuo yenu na kuuingiza katika mianzi ya pua zenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA. Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli, na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli. Kwa maana, angalia, yeye aifanyizaye milima, na kuuumba upepo, na kumwambia mwanadamu mawazo yake, afanyaye asubuhi kuwa giza, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka; BWANA, Mungu wa majeshi, ndilo jina lake.
Amosi 4:6-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Niliwapa njaa kwenye kila mji, na ukosefu wa chakula katika kila mji, hata hivyo bado hamjanirudia mimi,” asema BWANA. “Pia niliwazuilia ninyi mvua miezi mitatu kabla ya kufikia mavuno. Nilinyesha mvua kwenye mji mmoja, lakini niliizuia mvua isinyeshe mji mwingine. Shamba moja lilipata mvua, na lingine halikupata, nalo likakauka. Watu walitangatanga mji hata mji kutafuta maji, lakini hawakupata ya kuwatosha kunywa, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema BWANA. “Mara nyingi nilizipiga bustani zenu na mashamba ya mizabibu, niliyapiga kwa kutu na ukungu. Nzige walitafuna tini zenu na miti ya mizeituni, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema BWANA. “Niliwapelekea tauni miongoni mwenu kama nilivyofanya kule Misri. Niliwaua vijana wenu wa kiume kwa upanga, na nikawachukua farasi wenu. Nilijaza pua zenu kwa uvundo kutoka kambi zenu, hata hivyo hamjanirudia mimi,” asema BWANA. “Niliwaangamiza baadhi yenu kama nilivyoangamiza Sodoma na Gomora. Mlikuwa kama kijiti kiwakacho kilichonyakuliwa motoni, hata hivyo hamjanirudia,” asema BWANA. “Kwa hiyo hili ndilo nitakalowafanyia, Israeli, na kwa sababu nitawafanyia hili, jiandaeni kukutana na Mungu wenu, ee Israeli.” Yeye ambaye hufanya milima, anaumba upepo, na kufunua mawazo yake kwa mwanadamu, yeye ageuzaye asubuhi kuwa giza, na kukanyaga mahali pa juu pa nchi: BWANA Mungu wa majeshi ndilo jina lake.