Amosi 4:1-5
Amosi 4:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikilizeni neno hili, enyi wanawake ng'ombe wa Bashani mlioko huko mlimani Samaria; nyinyi mnaowaonea wanyonge, mnaowakandamiza maskini, na kuwaambia waume zenu: “Tuleteeni divai tunywe!” Sikilizeni ujumbe huu: Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu Mtakatifu nimeapa: “Tazama, siku zaja, ambapo watu watawakokoteni kwa kulabu, kila mmoja wenu kama samaki kwenye ndoana. Mtaburutwa hadi ukutani palipobomolewa, na kutupwa nje. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. “Enyi Waisraeli, nendeni basi huko Betheli mkaniasi! Nendeni Gilgali mkalimbikize makosa yenu! Toeni sadaka zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu. Toeni tambiko ya shukrani ya mikate iliyochachushwa. Tangazeni popote kwamba mmetoa kwa hiari; kwani ndivyo mnavyopenda kufanya! Mimi Bwana Mungu nimenena.
Amosi 4:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lisikieni neno hili, enyi ng'ombe wa Bashani, mnaokaa juu ya mlima wa Samaria, mnaowaonea maskini, na kuwaponda wahitaji; mnaowaambia bwana zao, Haya! Leteni, tunywe. Bwana MUNGU ameapa kwa utakatifu wake, ya kuwa, tazama, siku zitawajia, watakapowaondoa ninyi kwa kulabu, na mabaki yenu kwa ndoana. Nanyi mtatoka kwenye mahali palipobomolewa, kila mwanamke moja kwa moja mbele yake; nanyi mtajitupa katika Harmoni, asema BWANA. Njooni Betheli, mkakose; njoni Gilgali, mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu; mkachome sadaka ya shukrani, ya kitu kilichotiwa chachu; mkatangaze sadaka mtoazo kwa hiari na kuzihubiri habari zake; kwa maana ndivyo viwapendezavyo ninyi, enyi wana wa Israeli, asema Bwana MUNGU.
Amosi 4:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lisikieni neno hili, enyi ng’ombe wa Bashani, mnaokaa juu ya mlima wa Samaria, mnaowaonea maskini, na kuwaponda wahitaji; mnaowaambia bwana zao, Haya! Leteni, tunywe. Bwana MUNGU ameapa kwa utakatifu wake, ya kuwa, tazama, siku zitawajilia, watakapowaondoa ninyi kwa kulabu, na mabaki yenu kwa ndoana. Nanyi mtatoka kwenye mahali palipobomolewa, kila mwanamke moja kwa moja mbele yake; nanyi mtajitupa katika Harmoni, asema BWANA. Njoni Betheli, mkakose; njoni Gilgali, mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu; mkachome sadaka ya shukrani, ya kitu kilichotiwa chachu; mkatangaze sadaka mtoazo kwa hiari na kuzihubiri habari zake; kwa maana ndivyo viwapendezavyo ninyi, enyi wana wa Israeli, asema Bwana MUNGU.
Amosi 4:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sikilizeni neno hili, ninyi ngʼombe wa Bashani mlioko juu ya Mlima Samaria, ninyi wanawake mnaowadhulumu maskini, na kuwagandamiza wahitaji, na kuwaambia wanaume wenu, “Tuleteeni vinywaji!” BWANA Mwenyezi ameapa kwa utakatifu wake: “Hakika wakati utakuja mtakapochukuliwa na kulabu, na wanaosalia kwa ndoana za samaki. Nanyi mtaenda moja kwa moja kupitia mahali palipobomolewa kwenye ukuta, nanyi mtatupwa nje kuelekea Harmoni,” asema BWANA. “Nendeni Betheli mkatende dhambi; nendeni Gilgali mkazidi kutenda dhambi. Leteni dhabihu zenu kila asubuhi, zaka zenu kila mwaka wa tatu. Mchome mkate uliotiwa chachu kama sadaka ya shukrani, jisifuni kuhusu sadaka zenu za hiari: jigambeni kwa ajili ya sadaka hizo, enyi Waisraeli, kwa kuwa hili ndilo mnalopenda kulitenda,” asema BWANA Mwenyezi.