Amosi 3:1-15
Amosi 3:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Enyi Waisraeli, sikilizeni neno Mwenyezi-Mungu alilosema dhidi yenu, enyi taifa zima alilolitoa nchini Misri: “Kati ya mataifa yote ulimwenguni, ni nyinyi tu niliowachagua. Kwa hiyo nitawaadhibu nyinyi, kwa sababu ya uovu wenu wote.” Je, watu wawili huanza safari pamoja, bila ya kufanya mpango pamoja kwanza? Je, simba hunguruma porini kama hajapata mawindo? Je, mwanasimba hunguruma pangoni mwake kama hajakamata kitu? Je, mtego bila chambo utamnasa ndege? Je, mtego hufyatuka bila kuguswa na kitu? Je, baragumu ya vita hulia mjini bila kutia watu hofu? Je, mji hupatwa na janga asilolileta Mungu? Hakika, Bwana Mwenyezi-Mungu hafanyi kitu bila kuwafunulia watumishi wake manabii nia yake. Simba akinguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana Mwenyezi-Mungu akinena, ni nani atakataa kuutangaza ujumbe wake? Tangazeni katika ikulu za Ashdodi, na katika ikulu za nchi ya Misri: “Kusanyikeni kwenye milima inayoizunguka nchi ya Samaria, mkajionee msukosuko mkubwa na dhuluma zinazofanyika humo.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu hawa wameyajaza majumba yao vitu vya wizi na unyang'anyi. Hawajui kabisa kutenda yaliyo sawa! Kwa hiyo, adui ataizingira nchi yao, atapaharibu mahali pao pa kujihami, na kuziteka nyara ikulu zao.” Mwenyezi-Mungu, asema hivi: “Kama vile mchungaji ampokonyavyo simba kinywani miguu miwili tu au kipande cha sikio la kondoo, ndivyo watakavyonusurika watu wachache tu wa Israeli wakaao Samaria, ambao sasa wanalalia vitanda vizuri na matandiko ya hariri.” Bwana Mungu wa majeshi asema hivi: “Sikilizeni, mkawaonye wazawa wa Yakobo: Siku nitakapowaadhibu Waisraeli kwa sababu ya makosa yao, nitayaharibu pia madhabahu ya mji wa Betheli. Nitazikata pembe za kila madhabahu na kuziangusha chini. Nitaziharibu nyumba zote mjini na vijijini; nitazibomoa nyumba zilizopambwa kwa pembe, majumba makubwamakubwa hayatasalia hata moja. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Amosi 3:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lisikieni neno hili alilolisema BWANA juu yenu, enyi wana wa Israeli, juu ya jamaa yote niliowapandisha kutoka nchi ya Misri, nikisema, Ni ninyi tu niliowajua katika jamaa zote zilizo duniani; kwa sababu hiyo nitawapatiliza ninyi maovu yenu yote. Je! Watu wawili wanaweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? Je! Simba atanguruma mwituni, asipokuwa na mawindo? Mwanasimba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu? Je! Ndege ataanguka mtegoni juu ya nchi, mahali asipotegewa tanzi? Mtego utafyatuka juu ya nchi, bila kunasa kitu chochote? Je! Tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope? Mji utapatikana na hali mbaya, asiyoileta BWANA? Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana MUNGU amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri? Tangazeni habari katika majumba ya Ashdodi, na katika majumba ya nchi ya Misri, mkaseme, Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria, katazameni, ni mishindo mikubwa kama nini iliyomo humo, na udhalimu mwingi kama nini uliomo ndani yake. Kwa maana hawajui kutenda haki, asema BWANA, hao wawekao akiba ya jeuri na unyang'anyi katika majumba yao. Basi, haya ndiyo asemayo Bwana MUNGU; Atakuwako adui, kuizunguka nchi pande zote; naye atazishusha chini nguvu zako zikutoke; na majumba yako yatatekwa nyara. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kama vile mchungaji apokonyavyo kinywani mwa simba miguu miwili, au kipande cha sikio; ndivyo watakavyopokonywa wana wa Israeli, wakaao Samaria katika pembe ya kochi, na juu ya mito ya hariri ya kitanda. Sikieni, mkashuhudu juu ya nyumba ya Yakobo, asema Bwana, MUNGU wa majeshi. Kwani katika siku ile nitakapompatiliza Israeli makosa yake, nitazipatiliza pia madhabahu za Betheli, na pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali, na kuanguka chini. Nami nitaipiga nyumba ya wakati wa baridi pamoja na nyumba ya wakati wa joto; na hizo nyumba za pembe zitaangamia, nazo nyumba kubwa zitakuwa na mwisho, asema BWANA.
Amosi 3:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lisikieni neno hili alilolisema BWANA juu yenu, enyi wana wa Israeli, juu ya jamaa yote niliowapandisha kutoka nchi ya Misri, nikisema, Ni ninyi tu niliowajua katika jamaa zote zilizo duniani; kwa sababu hiyo nitawapatiliza ninyi maovu yenu yote. Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? Je! Simba atanguruma mwituni, asipokuwa na mawindo? Mwana-simba atalia pangoni mwake, ikiwa hakupata kitu? Je! Ndege ataanguka mtegoni juu ya nchi, mahali asipotegewa tanzi? Mtego utafyatuka juu ya nchi, bila kunasa kitu cho chote? Je! Tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope? Mji utapatikana na hali mbaya, asiyoileta BWANA? Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. Simba amekwisha kunguruma, ni nani asiyeogopa? Bwana MUNGU amenena, ni nani awezaye neno ila kutabiri? Tangazeni habari katika majumba ya Ashdodi, na katika majumba ya nchi ya Misri, mkaseme, Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria, katazameni, ni mishindo mikubwa kama nini iliyomo humo, na udhalimu mwingi kama nini uliomo ndani yake. Kwa maana hawajui kutenda haki, asema BWANA, hao wawekao akiba ya jeuri na unyang’anyi katika majumba yao. Basi, haya ndiyo asemayo Bwana MUNGU; Atakuwako adui, kuizunguka nchi pande zote; naye atazishusha chini nguvu zako zikutoke; na majumba yako yatatekwa nyara. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kama vile mchungaji apokonyavyo kinywani mwa simba miguu miwili, au kipande cha sikio; ndivyo watakavyopokonywa wana wa Israeli, wakaao Samaria katika pembe ya semadari, na juu ya mito ya hariri ya kitanda. Sikieni, mkashuhudu juu ya nyumba ya Yakobo, asema Bwana, MUNGU wa majeshi. Kwani katika siku ile nitakapompatiliza Israeli makosa yake, nitazipatiliza pia madhabahu za Betheli, na pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali, na kuanguka chini. Nami nitaipiga nyumba ya wakati wa baridi pamoja na nyumba ya wakati wa hari; na hizo nyumba za pembe zitaangamia, nazo nyumba kubwa zitakuwa na mwisho, asema BWANA.
Amosi 3:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sikilizeni neno hili alilosema BWANA dhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri: “Ni ninyi tu niliowachagua kati ya jamaa zote za dunia; kwa hiyo nitawaadhibu kwa ajili ya dhambi zenu zote.” Je, watu wawili hutembea pamoja wasipokubaliana kufanya hivyo? Je, simba hunguruma katika kichaka wakati hana mawindo? Aweza kuvuma katika pango wakati ambao hajakamata chochote? Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini ambapo hajategewa chambo? Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini wakati hakuna chochote cha kunasa? Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari, watu hawatetemeki? Mji unapopatwa na maafa, je, si BWANA amesababisha? Hakika BWANA Mwenyezi hatafanya neno lolote bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. Simba amenguruma: je, ni nani ambaye hataogopa? BWANA Mwenyezi ametamka: je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii? Tangazeni katika ngome za Ashdodi na katika ngome za Misri: “Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria; angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake, na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.” BWANA asema: “Hawajui kutenda lililo jema, wale ambao hujilundikia nyara na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.” Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: “Adui ataizingira nchi; ataangusha chini ngome zenu na kuteka nyara maboma yenu.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba vipande viwili tu vya mfupa wa mguu au kipande cha sikio, hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa, wale wanaokaa Samaria kwenye kingo za vitanda vyao, na katika Dameski kwenye viti vyao vya fahari.” “Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana, BWANA Mungu wa majeshi. “Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake, nitaharibu madhabahu za Betheli; pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali na kuanguka chini. Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika, pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi; nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,” asema BWANA.