Amosi 2:6-16
Amosi 2:6-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Waisraeli wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Wamewauza watu waaminifu kwa kuwa hawakuweza kulipa madeni yao; na kuwauza watu fukara wasioweza kulipa deni la kandambili. Huwanyanyasa na kuwakandamiza wanyonge, na maskini huwabagua wasipate haki zao. Mtu na baba yake hulala na mjakazi yuleyule, hivyo hulitia unajisi jina langu takatifu. Popote penye madhabahu, watu hulalia nguo walizotwaa kwa maskini kama dhamana ya madeni yao; na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai waliyotwaa kwa wadeni wao. “Hata hivyo, enyi watu wangu, kwa ajili yenu, niliwaangamiza kabisa Waamori ambao walikuwa wakubwa kama mierezi, wenye nguvu kama miti ya mialoni. Naam, niliwaangamiza, matawi na mizizi. Niliwatoeni kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza kupitia jangwani miaka arubaini, mpaka mkaichukua nchi ya Waamori kuwa yenu. Niliwateua baadhi ya wana wenu wawe manabii, na baadhi ya vijana wenu wawe wanadhiri. Je, enyi Waisraeli, haya nisemayo si ya kweli? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Lakini nyinyi mliwafanya wanadhiri wanywe divai, na kuwaamuru manabii wasitoe unabii. “Sasa basi, nitawagandamiza mpaka chini, kama gari lililojaa nafaka. Hata wapiga mbio hodari hawataweza kutoroka; wenye nguvu wataishiwa nguvu zao, na askari watashindwa kuyaokoa maisha yao. Wapiga upinde vitani hawatastahimili; wapiga mbio hodari hawataweza kujiokoa, wala wapandafarasi hawatayanusurisha maisha yao. Siku hiyo, hata askari hodari watatimua mbio bila chochote. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Amosi 2:6-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu; nao hukanyaga vichwa vya maskini katika mavumbi ya nchi na kuwasukuma walioteseka kutoka kwa njia yao; na mtu na baba yake wanamwendea mwanamke mmoja, na kulitia unajisi jina langu takatifu; nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha. Lakini nilimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini niliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini. Pia niliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arubaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya Mwamori. Nami nikawainua watu miongoni mwa wana wenu wawe manabii, na katika vijana wenu wawe Wanadhiri; je! Sivyo hivyo, enyi wana wa Israeli? Asema BWANA. Lakini mliwapa Wanadhiri mvinyo wanywe; mkawaamuru manabii, mkisema, Msifanye unabii. Tazameni, nitawalemea ninyi, Kama gari lilemeavyo lililojaa miganda. Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; Wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; Wala shujaa hatajiokoa nafsi yake; Wala apindaye upinde hatasimama; Wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; Wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake; Naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa Atakimbia uchi siku ile, asema BWANA.
Amosi 2:6-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu; nao hutwetea mavumbi yaliyo juu ya vichwa vya maskini, na kuipotosha njia ya mwenye upole; na mtu na baba yake humwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina langu takatifu; nao hujilaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha. Lakini nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini. Pia naliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arobaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya Mwamori. Nami nikawainua watu miongoni mwa wana wenu wawe manabii, na katika vijana wenu wawe Wanadhiri; je! Sivyo hivyo, enyi wana wa Israeli? Asema BWANA. Lakini mliwapa Wanadhiri mvinyo wanywe; mkawaamuru manabii, mkisema, Msifanye unabii. Tazameni, nitawalemea ninyi, Kama gari lilemeavyo lililojaa miganda. Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; Wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; Wala shujaa hatajiokoa nafsi yake; Wala apindaye upinde hatasimama; Wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; Wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake; Naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa Atakimbia uchi siku ile, asema BWANA.
Amosi 2:6-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Israeli, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Wanawauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu. Wanakanyaga juu ya vichwa vya maskini, kama vile juu ya mavumbi ya nchi, na kukataa haki kwa waliodhulumiwa. Baba na mwanawe hushiriki msichana mmoja, kwa hivyo hulinajisi Jina langu takatifu. Watu hulala kando ya kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani. Katika nyumba ya mungu wao hunywa mvinyo ulionunuliwa kwa fedha walizotozwa watu. “Nilimwangamiza Mwamori mbele yao, ingawa alikuwa mrefu kama mierezi, na mwenye nguvu kama mialoni. Niliyaangamiza matunda yake juu na mizizi yake chini. “Niliwapandisha toka Misri, na nikawaongoza miaka arobaini jangwani niwape nchi ya Waamori. “Pia niliinua manabii kutoka miongoni mwa wana wenu na Wanadhiri kutoka miongoni mwa vijana wenu. Je, hii si kweli, enyi watu wa Israeli?” asema BWANA. “Lakini mliwafanya Wanadhiri kunywa mvinyo na kuwaamuru manabii wasitoe unabii. “Sasa basi, nitawaponda kama gari linavyoponda likiwa limejazwa nafaka. Mkimbiaji hodari hatanusurika, wenye nguvu wataishiwa nguvu zao, na shujaa hataweza kuokoa maisha yake. Mpiga upinde atakimbia, askari wapiga mbio hawataweza kutoroka, na mpanda farasi hataokoa maisha yake. Hata askari walio mashujaa sana siku hiyo watakimbia uchi,” asema BWANA.