Amosi 1:1-15
Amosi 1:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Maneno ya Amosi, mmojawapo wa wachungaji wa mji wa Tekoa. Mungu alimfunulia Amosi mambo haya yote kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya lile tetemeko la ardhi, wakati Uzia alipokuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yoashi, alipokuwa mfalme wa Israeli. Amosi alisema hivi: Mwenyezi-Mungu ananguruma kutoka mlima Siyoni, anavumisha sauti yake kutoka Yerusalemu, hata malisho ya wachungaji yanakauka, nyasi mlimani Karmeli zinanyauka. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Damasko wametenda dhambi tena na tena; kwa hiyo, sitaacha kuwaadhibu; waliwatendea watu wa Gileadi ukatili mbaya. Basi, nitaishushia moto ikulu ya mfalme Hazaeli, nao utaziteketeza kabisa ngome za mfalme Ben-hadadi. Nitayavunjavunja malango ya mji wa Damasko, na kuwang'oa wakazi wa bonde la Aweni, pamoja na mtawala wa Beth-edeni. Watu wa Aramu watapelekwa uhamishoni Kiri. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Gaza wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Walichukua mateka watu kabila zima, wakawauza wawe watumwa kwa Waedomu. Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Gaza, nao utaziteketeza kabisa ngome zake. Nitawang'oa wakazi wa mji wa Ashdodi, pamoja na mtawala wa Ashkeloni. Nitanyosha mkono dhidi ya Ekroni, nao Wafilisti wote waliosalia wataangamia. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Tiro wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Walichukua mateka kabila zima hadi Edomu, wakaukiuka mkataba wa urafiki waliokuwa wamefanya. Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Tiro, na kuziteketeza kabisa ngome zake.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Edomu wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Waliwawinda ndugu zao Waisraeli kwa mapanga, wakaitupilia mbali huruma yao yote ya kindugu. Hasira yao haikuwa na kikomo, waliiacha iwake daima. Basi, nitaushushia moto mji wa Temani, na kuziteketeza kabisa ngome za Bosra.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Watu wa Amoni wametenda dhambi tena na tena, kwa hiyo sitaacha kuwaadhibu. Katika vita vyao vya kupora nchi zaidi, waliwatumbua wanawake waja wazito nchini Gileadi. Basi, nitazishushia moto kuta za mji wa Raba, na kuziteketeza kabisa ngome zake. Siku hiyo ya vita patakuwa na makelele mengi, nayo mapambano yatakuwa makali kama tufani. Mfalme wao na maofisa wake, wote watakwenda kukaa uhamishoni. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Amosi 1:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi. Naye alisema, BWANA atanguruma toka Sayuni, Atatoa sauti yake toka Yerusalemu; Na malisho ya wachungaji yatakauka, Na kilele cha Karmeli kitanyauka. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma; lakini nitatuma moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi. Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda uhamishoni hadi Kiri, asema BWANA. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Gaza, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu waiiteka nyara kabila nzima, wawatie katika mikono ya Edomu; lakini nitatuma moto juu ya ukuta wa Gaza, nao utayateketeza majumba yake. Nami nitamkatilia mbali mwenyeji katika Ashdodi; na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Ashkeloni; nami nitaugeuza mkono wangu uwe juu ya Ekroni; na mabaki ya Wafilisti wataangamia, asema Bwana MUNGU. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Tiro, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameitia kabila nzima katika mikono ya Edomu, wala hawakulikumbuka agano la udugu; lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Tiro, nao utayateketeza majumba yake. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Edomu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, akatupilia mbali huruma zake zote; hasira yake ikararuararua daima, akaishika ghadhabu yake milele; lakini nitatuma moto juu ya Temani, nao utayateketeza majumba ya Bosra. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya wana wa Amoni, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewapasua wanawake wa Gileadi wenye mimba, ili wapate kuongeza mipaka yao; lakini nitawasha moto katika ukuta wa Raba, nao utayateketeza majumba yake; pamoja na kupiga kelele siku ya vita, pamoja na tufani katika siku ya chamchela; na mfalme wao atakwenda utumwani, yeye na wakuu wake wote pamoja, asema BWANA.
Amosi 1:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi. Naye alisema, BWANA atanguruma toka Sayuni, Atatoa sauti yake toka Yerusalemu; Na malisho ya wachungaji yataomboleza, Na kilele cha Karmeli kitanyauka. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma; lakini nitapeleka moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi. Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda hali ya kufungwa hata Kiri, asema BWANA. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Gaza, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu waliichukua katika hali ya kufungwa kabila nzima, wawatie katika mikono ya Edomu; lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Gaza, nao utayateketeza majumba yake. Nami nitamkatilia mbali mwenyeji katika Ashdodi; na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Ashkeloni; nami nitaugeuza mkono wangu uwe juu ya Ekroni; na mabaki ya Wafilisti wataangamia, asema Bwana MUNGU. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Tiro, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameitia kabila nzima katika mikono ya Edomu, wala hawakulikumbuka agano la udugu; lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Tiro, nao utayateketeza majumba yake. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya Edomu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, akatupilia mbali huruma zake zote; hasira yake ikararua-rarua daima, akaishika ghadhabu yake milele; lakini nitapeleka moto juu ya Temani, nao utayateketeza majumba ya Bosra. Haya ndiyo asemayo BWANA; Kwa makosa matatu ya wana wa Amoni, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewapasua wanawake wa Gileadi wenye mimba, ili wapate kuongeza mipaka yao; lakini nitawasha moto katika ukuta wa Raba, nao utayateketeza majumba yake; pamoja na kupiga kelele siku ya vita, pamoja na tufani katika siku ya chamchela; na mfalme wao atakwenda utumwani, yeye na wakuu wake wote pamoja, asema BWANA.
Amosi 1:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Maneno ya Amosi, mmoja wa wachungaji wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli. Alisema: “BWANA ananguruma toka Sayuni, pia ananguruma kutoka Yerusalemu; malisho ya wachungaji yanakauka, kilele cha Karmeli kinanyauka.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Dameski, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliipura Gileadi kwa vyombo vya chuma vyenye meno. Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi. Nitalivunja lango la Dameski; nitamwangamiza mfalme aliye katika Bonde la Aveni, na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni. Watu wote wa Aramu wataenda uhamishoni huko Kiri,” asema BWANA. Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Gaza, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu walichukua mateka jumuiya nzima na kuwauza kwa Edomu, nitatuma moto juu ya kuta za Gaza ambao utateketeza ngome zake. Nitamwangamiza mfalme wa Ashdodi na yeye aishikaye fimbo ya utawala katika Ashkeloni. Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni, hadi Mfilisti wa mwisho atakapokufa,” asema BWANA Mwenyezi. Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Tiro, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu ameuza jumuiya nzima ya mateka kwa Edomu, na kutokujali mapatano ya undugu, Nitatuma moto kwenye kuta za Tiro ambao utateketeza ngome zake.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Edomu, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, alikataa kuonesha huruma yoyote, kwa sababu hasira yake kali iliendelea kupanda wakati wote na ghadhabu iliwaka bila kuzuiliwa. Nitatuma moto juu ya Temani ambao utateketeza ngome za Bosra.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Amoni, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu aliwatumbua wanawake wajawazito wa Gileadi ili kuongeza mipaka yake. Nitatuma moto kwenye kuta za Raba ambao utateketeza ngome zake katikati ya kelele za vita katika siku ya mapigano, katikati ya upepo mkali katika siku ya dhoruba. Mfalme wake ataenda uhamishoni, yeye pamoja na maafisa wake,” asema BWANA.