Matendo 9:19-31
Matendo 9:19-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko. Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, “Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!” Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa. Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi walikusanyika na kufanya mpango wa kumuua Saulo. Lakini Saulo alipata habari ya mpango huo. Usiku na mchana walilinda milango ya kuingia mjini ili wapate kumuua. Lakini wakati wa usiku wanafunzi wake walimchukua, wakamteremsha chini ndani ya kapu kubwa kwa kupitia nafasi iliyokuwako ukutani. Saulo alipofika Yerusalemu alijaribu kujiunga na wale wanafunzi. Lakini wote walimwogopa hawakuweza kuamini kwamba yeye amekuwa mfuasi. Hapo, Barnaba alikuja akamchukua Saulo, akampeleka kwa mitume na kuwaeleza jinsi Saulo alivyomwona Bwana njiani na jinsi Bwana alivyoongea naye. Aliwaambia pia jinsi Saulo alivyokuwa amehubiri bila woga kule Damasko. Basi, Saulo alikaa pamoja nao, akatembelea Yerusalemu yote akihubiri neno la Bwana bila hofu. Pia aliongea na kubishana na Wayahudi wanaoongea Kigiriki, lakini wao walijaribu kumwua. Wale ndugu walipogundua jambo hilo, walimchukua Saulo, wakampeleka Kaisarea, wakamwacha aende zake Tarso. Wakati huo kanisa likawa na amani popote katika Yudea, Galilaya, na Samaria. Lilijengwa na kukua katika kumcha Bwana, na kuongezeka likitiwa moyo na Roho Mtakatifu.
Matendo 9:19-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadhaa pamoja na wanafunzi walioko Dameski. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaua walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue; lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua. Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimteremsha katika kapu. Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kigiriki. Nao wakajaribu kumwua. Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakamtuma aende Tarso. Basi kanisa likapata raha kote katika Yudea na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.
Matendo 9:19-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue; lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua. Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu. Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua. Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso. Basi kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.
Matendo 9:19-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski. Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?” Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo. Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakapanga njama kumuua Sauli. Lakini Sauli akagundua njama yao. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, usiku na mchana ili wapate kumuua. Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani. Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi. Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski. Kwa hiyo Sauli akakaa nao akitembea kwa uhuru kila mahali huko Yerusalemu, akihubiri kwa ujasiri katika jina la Bwana. Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani, lakini wao walijaribu kumuua. Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso. Ndipo kanisa katika Yudea yote, Galilaya na Samaria likawa na wakati wa amani. Likatiwa nguvu; na kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, idadi yake ikaongezeka, na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana.