Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 9:18-43

Matendo 9:18-43 Biblia Habari Njema (BHN)

Mara vitu kama magamba vikaanguka kutoka machoni mwa Saulo, akaweza kuona tena. Akasimama, akabatizwa. Na baada ya kula chakula, nguvu zake zikamrudia. Saulo alikaa siku chache pamoja na wafuasi huko Damasko. Mara alianza kuhubiri katika masunagogi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, “Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!” Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa. Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi walikusanyika na kufanya mpango wa kumuua Saulo. Lakini Saulo alipata habari ya mpango huo. Usiku na mchana walilinda milango ya kuingia mjini ili wapate kumuua. Lakini wakati wa usiku wanafunzi wake walimchukua, wakamteremsha chini ndani ya kapu kubwa kwa kupitia nafasi iliyokuwako ukutani. Saulo alipofika Yerusalemu alijaribu kujiunga na wale wanafunzi. Lakini wote walimwogopa hawakuweza kuamini kwamba yeye amekuwa mfuasi. Hapo, Barnaba alikuja akamchukua Saulo, akampeleka kwa mitume na kuwaeleza jinsi Saulo alivyomwona Bwana njiani na jinsi Bwana alivyoongea naye. Aliwaambia pia jinsi Saulo alivyokuwa amehubiri bila woga kule Damasko. Basi, Saulo alikaa pamoja nao, akatembelea Yerusalemu yote akihubiri neno la Bwana bila hofu. Pia aliongea na kubishana na Wayahudi wanaoongea Kigiriki, lakini wao walijaribu kumwua. Wale ndugu walipogundua jambo hilo, walimchukua Saulo, wakampeleka Kaisarea, wakamwacha aende zake Tarso. Wakati huo kanisa likawa na amani popote katika Yudea, Galilaya, na Samaria. Lilijengwa na kukua katika kumcha Bwana, na kuongezeka likitiwa moyo na Roho Mtakatifu. Petro alipokuwa anasafirisafiri kila mahali alifika pia kwa watu wa Mungu waliokuwa wanaishi Luda. Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea ambaye kwa muda wa miaka minane alikuwa amelala kitandani kwa sababu alikuwa amepooza. Basi, Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya. Amka utandike kitanda chako.” Ainea akaamka mara. Wakazi wote wa Luda na Saroni walimwona Ainea, na wote wakamgeukia Bwana. Kulikuwa na mfuasi mmoja mwanamke mjini Yopa aitwaye Tabitha (kwa Kigiriki ni Dorka, maana yake, Paa). Huyo mwanamke alikuwa akitenda mema na kuwasaidia maskini daima. Wakati huo ikawa kwamba aliugua, akafa. Watu wakauosha mwili wake, wakaulaza katika chumba ghorofani. Yopa si mbali sana na Luda; kwa hiyo wafuasi waliposikia kwamba Petro alikuwa Luda, wakawatuma watu wawili kwake na ujumbe: “Njoo kwetu haraka iwezekanavyo.” Basi, Petro akaenda pamoja nao. Alipofika alipelekwa ghorofani katika kile chumba. Huko wajane wengi walimzunguka Petro wakilia na kumwonesha makoti na nguo ambazo Dorka alikuwa akitengeneza wakati alipokuwa hai. Petro aliwatoa nje wote, akapiga magoti, akasali. Kisha akaigeukia ile maiti, akasema, “Tabitha, amka.” Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro, akaketi. Petro akamsaidia kusimama, halafu akawaita wale watu wa Mungu na wale wajane, akamkabidhi kwao akiwa mzima. Habari za tukio hili zilienea kila mahali huko Yopa, na watu wengi wakamwamini Bwana. Petro alikaa siku kadhaa huko Yopa, akiishi kwa mtu mmoja mtengenezaji wa ngozi aitwaye Simoni.

Shirikisha
Soma Matendo 9

Matendo 9:18-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa; akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadhaa pamoja na wanafunzi walioko Dameski. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaua walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue; lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua. Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimteremsha katika kapu. Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kigiriki. Nao wakajaribu kumwua. Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakamtuma aende Tarso. Basi kanisa likapata raha kote katika Yudea na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. Wakati Petro alipokuwa akizungukazunguka pande zote akawateremkia na watakatifu waliokaa Lida. Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo alikuwa amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; inuka, ujitandikie. Mara akainuka. Na watu wote waliokaa Lida na Sharoni wakamwona, wakamgeukia Bwana. Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; wakati walipokwisha kumwosha, wakamweka ghorofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi waliosikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Njoo kwetu pasipo kukawia. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu ghorofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, inuka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua; hata kisha akawaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, akiwa hai. Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana. Basi Petro akakaa siku kadhaa huko Yafa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi.

Shirikisha
Soma Matendo 9

Matendo 9:18-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa; akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani? Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamwue; lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumwua. Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu. Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua. Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso. Basi kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. Hata Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote akawatelemkia na watakatifu waliokaa Lida. Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka. Na watu wote waliokaa Lida na Sharoni wakamwona, wakamgeukia Bwana. Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana. Basi Petro akakaa siku kadha wa kadha huko Yafa, nyumbani mwa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi.

Shirikisha
Soma Matendo 9

Matendo 9:18-43 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa. Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski. Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?” Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo. Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakapanga njama kumuua Sauli. Lakini Sauli akagundua njama yao. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, usiku na mchana ili wapate kumuua. Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani. Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi. Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski. Kwa hiyo Sauli akakaa nao akitembea kwa uhuru kila mahali huko Yerusalemu, akihubiri kwa ujasiri katika jina la Bwana. Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani, lakini wao walijaribu kumuua. Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso. Ndipo kanisa katika Yudea yote, Galilaya na Samaria likawa na wakati wa amani. Likatiwa nguvu; na kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, idadi yake ikaongezeka, na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana. Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alienda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida. Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, aliyekuwa amepooza na kwa muda wa miaka nane alikuwa hajatoka kitandani. Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka. Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana. Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini. Wakati huo akaugua, akafa, na wakauosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani. Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.” Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao. Alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai. Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana. Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.

Shirikisha
Soma Matendo 9