Matendo 8:1-40
Matendo 8:1-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Saulo naye alikiona kitendo hicho cha kumwua kuwa sawa. Siku hiyo kanisa la Yerusalemu lilianza kuteswa vibaya. Waumini wote, isipokuwa tu wale mitume, walilazimika kutawanyika katika sehemu za mashambani za Yudea na Samaria. Watu wamchao Mungu walimzika Stefano na kumfanyia maombolezo makubwa. Wakati huohuo, Saulo alijaribu kuliangamiza kanisa. Alikwenda katika kila nyumba, akawatoa nje waumini, wanaume kwa wanawake, akawatia gerezani. Wale waumini waliotawanyika, walikwenda kila mahali wakihubiri ule ujumbe. Naye Filipo aliingia katika mji wa Samaria na kumhubiri Kristo kwa wenyeji wa hapo. Watu walijiunga kusikiliza kwa makini ule ujumbe wa Filipo na kuona ile miujiza aliyoifanya. Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa. Kukawa na furaha kubwa katika mji ule. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni ambaye alikuwa amekwisha fanya uchawi wake katika mji huo kwa muda na kuwashangaza watu wa Samaria, akijiona kuwa yeye ni mtu maarufu. Watu wote, wadogo kwa wakubwa, walimsikiliza kwa makini wakisema, “Simoni ndiye nguvu ya kimungu inayoitwa ‘Nguvu Kubwa.’” Walivutiwa sana naye kwa vile alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake kwa muda mrefu. Lakini walipouamini ujumbe wa Filipo juu ya Habari Njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, walibatizwa, wanawake na wanaume. Hata Simoni aliamini; na baada ya kubatizwa alikuwa akiandamana na Filipo, akastaajabia maajabu na miujiza iliyokuwa inafanyika. Wale mitume waliokuwa kule Yerusalemu walipopata habari kwamba wenyeji wa Samaria nao wamelipokea neno la Mungu, waliwatuma huko Petro na Yohane. Walipofika waliwaombea hao waumini ili wampokee Roho Mtakatifu; maana wakati huo Roho Mtakatifu hakuwa amemshukia yeyote kati yao; walikuwa wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu. Basi, Petro na Yohane wakawawekea mikono hao waumini, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hapo Simoni alingamua kwamba kwa kuwekewa mikono ya mitume waumini walipewa Roho Mtakatifu. Hivyo aliwapa Petro na Yohane fedha akisema, “Nipeni na mimi uwezo huo ili yeyote nitakayemwekea mikono, apokee Roho Mtakatifu.” Lakini Petro akamjibu, “Potelea mbali na fedha zako kwa vile unafikiri kwamba unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! Huna sehemu yoyote wala haki katika kazi hiyo kwa maana moyo wako hauko sawa mbele ya macho ya Mungu. Kwa hiyo, tubu ubaya wako huu na umwombe Bwana naye anaweza kukusamehe fikira kama hizo. Ni dhahiri kwangu kwamba umejaa wivu mkali na u mfungwa wa dhambi!” Simoni akajibu, “Tafadhali, niombeeni kwa Bwana lisije likanipata lolote kati ya hayo mliyosema.” Baada ya Petro na Yohane kutoa ushuhuda wao na kuutangaza ujumbe wa Bwana, walirudi Yerusalemu. Walipokuwa wanarudi walihubiri Habari Njema katika vijiji vingi vya Samaria. Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jitayarishe uende kusini kupitia njia inayotoka Yerusalemu kwenda Gaza.” (Njia hiyo hupita jangwani). Basi, Filipo akajiweka tayari, akaanza safari. Wakati huohuo kulikuwa na Mwethiopia mmoja, towashi, ambaye alikuwa anasafiri kuelekea nyumbani. Huyo mtu alikuwa mkurugenzi maarufu wa hazina ya Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa amekwenda huko Yerusalemu kuabudu na wakati huo alikuwa anarudi akiwa amepanda gari la kukokotwa. Alipokuwa anasafiri, alikuwa akijisomea kitabu cha nabii Isaya. Basi, Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda karibu na gari hilo ukafuatane nalo.” Filipo akakimbilia karibu na gari, akamsikia huyo mtu akisoma katika kitabu cha nabii Isaya. Hapo Filipo akamwuliza, “Je, unaelewa hayo unayosoma?” Huyo mtu akamjibu, “Ninawezaje kuelewa bila mtu kuniongoza?” Hapo akamwalika Filipo apande juu, aketi pamoja naye. Basi, sehemu ya Maandiko Matakatifu aliyokuwa anasoma ilikuwa hii: “Alikuwa kama kondoo anayepelekwa kuchinjwa; kimya kama vile mwanakondoo anapokatwa manyoya, yeye hakutoa sauti hata kidogo. Alifedheheshwa na kunyimwa haki. Hakuna atakayeweza kuongea juu ya kizazi chake, kwa maana maisha yake yameondolewa duniani.” Huyo Mwethiopia akamwambia Filipo, “Niambie, huyu nabii anasema juu ya nini? Anasema mambo haya juu yake yeye mwenyewe au juu ya mtu mwingine?” Basi, Filipo akianzia na sehemu hiyo ya Maandiko Matakatifu, akamweleza Habari Njema juu ya Yesu. Walipokuwa bado wanaendelea na safari, walifika mahali penye maji, na huyo ofisa akasema, “Mahali hapa pana maji; je, kuna chochote cha kunizuia nisibatizwe?” [ Filipo akasema, “Kama unaamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Naye akajibu, “Naam, ninaamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”] Basi, huyo ofisa akaamuru lile gari lisimame; na wote wawili, Filipo na huyo towashi wakashuka majini, naye Filipo akambatiza. Walipotoka majini Roho wa Bwana akamfanya Filipo atoweke. Na huyo towashi hakumwona tena; lakini akaendelea na safari yake mwenye furaha. Filipo akajikuta yuko Azoto, akapita katika miji yote akihubiri Injili mpaka alipofika Kaisarea.
Matendo 8:1-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile kukatokea mateso makuu kwa kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Yudea na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huku na huko wakilihubiri neno. Filipo akateremka akaingia katika mji wa Samaria, akawahubiria Kristo. Na mkutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, aliye Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri Habari Njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Wakati Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili ikiwezekana, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona uko katika uchungu kama nyongo, na tena uko katika kifungo cha uovu. Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikie mambo haya mliyosema hata moja. Nao walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria. Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile iteremkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyesimamia hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirudi nyumbani, akiwa ameketi garini mwake akisoma kitabu cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukaribiane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma kitabu cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake yule amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi. Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiria Habari Njema za Yesu. Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? [ Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] Akaamuru lile gari lisimame; wakateremka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi. Lakini Filipo akaonekana katika Azota, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hadi akafika Kaisaria.
Matendo 8:1-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu. Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja. Nao walipokwisha kushuhudia na kulihubiri neno la Bwana wakarudi Yerusalemu, wakaihubiri Injili katika vijiji vingi vya Wasamaria. Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi. Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu. Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? [ Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi. Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.
Matendo 8:1-40 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Naye Sauli alikua pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano. Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Yudea na Samaria. Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwomboleza sana. Lakini Sauli alianza kuliangamiza kanisa. Aliingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipoenda. Filipo akaenda mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo. Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza alizofanya, wakasikiliza kwa makini yale aliyosema. Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele, na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo. Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu, nao watu wote, wakubwa kwa wadogo, wakamsikiliza na kustaajabu, wakisema, “Mtu huyu ndiye ajulikanaye kama Uweza Mkuu wa Mungu.” Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake. Lakini watu walipomwamini Filipo akihubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona. Basi mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria wamelipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko. Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu, kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa bado hajawashukia hata mmoja ila wamebatizwa tu katika jina la Bwana Yesu. Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho Mtakatifu. Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho Mtakatifu mitume walipoweka mikono juu yao, akataka kuwapa fedha akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho Mtakatifu.” Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Bwana. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako. Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.” Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili hayo mliyosema lolote lisinitokee.” Nao walipokwisha kutoa ushuhuda na kuhubiri neno la Bwana, wakarudi Yerusalemu wakihubiri Injili katika vijiji vingi vya Samaria. Basi malaika wa Bwana akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara inayotoka Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.” Hivyo akaondoka. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa ameenda Yerusalemu ili kuabudu, naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi kwenye gari lake la vita akisoma kitabu cha nabii Isaya. Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.” Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamuuliza, “Je, unaelewa hayo unayoyasoma?” Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye. Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la Maandiko: “Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni, kama mwana-kondoo anyamazavyo mbele yake yule amkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake. Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake. Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake? Kwa maana maisha yake yaliondolewa kutoka duniani.” Yule towashi akamuuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?” Ndipo Filipo akaanza kutumia fungu lile la Maandiko, akamweleza Habari Njema ya Yesu. Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamuuliza Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?” [ Filipo akamwambia, “Ukiamini kwa moyo wako wote, unaweza kubatizwa.” Akajibu, “Naamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”] Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Filipo na yule towashi wakateremka kwenye maji pamoja, naye Filipo akambatiza. Nao walipotoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi. Filipo akajikuta Azoto; akasafiri akihubiri Injili katika miji yote hadi akafika Kaisaria.