Matendo 8:1-13
Matendo 8:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Saulo naye alikiona kitendo hicho cha kumwua kuwa sawa. Siku hiyo kanisa la Yerusalemu lilianza kuteswa vibaya. Waumini wote, isipokuwa tu wale mitume, walilazimika kutawanyika katika sehemu za mashambani za Yudea na Samaria. Watu wamchao Mungu walimzika Stefano na kumfanyia maombolezo makubwa. Wakati huohuo, Saulo alijaribu kuliangamiza kanisa. Alikwenda katika kila nyumba, akawatoa nje waumini, wanaume kwa wanawake, akawatia gerezani. Wale waumini waliotawanyika, walikwenda kila mahali wakihubiri ule ujumbe. Naye Filipo aliingia katika mji wa Samaria na kumhubiri Kristo kwa wenyeji wa hapo. Watu walijiunga kusikiliza kwa makini ule ujumbe wa Filipo na kuona ile miujiza aliyoifanya. Maana pepo wachafu waliokuwa wamewapagaa watu wengi waliwatoka wakipiga kelele kubwa; na pia watu wengi waliokuwa wamepooza viungo na waliolemaa waliponywa. Kukawa na furaha kubwa katika mji ule. Basi, kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Simoni ambaye alikuwa amekwisha fanya uchawi wake katika mji huo kwa muda na kuwashangaza watu wa Samaria, akijiona kuwa yeye ni mtu maarufu. Watu wote, wadogo kwa wakubwa, walimsikiliza kwa makini wakisema, “Simoni ndiye nguvu ya kimungu inayoitwa ‘Nguvu Kubwa.’” Walivutiwa sana naye kwa vile alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake kwa muda mrefu. Lakini walipouamini ujumbe wa Filipo juu ya Habari Njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, walibatizwa, wanawake na wanaume. Hata Simoni aliamini; na baada ya kubatizwa alikuwa akiandamana na Filipo, akastaajabia maajabu na miujiza iliyokuwa inafanyika.
Matendo 8:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku ile kukatokea mateso makuu kwa kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Yudea na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huku na huko wakilihubiri neno. Filipo akateremka akaingia katika mji wa Samaria, akawahubiria Kristo. Na mkutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, aliye Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri Habari Njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.
Matendo 8:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.
Matendo 8:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Naye Sauli alikua pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano. Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Yudea na Samaria. Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwomboleza sana. Lakini Sauli alianza kuliangamiza kanisa. Aliingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipoenda. Filipo akaenda mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo. Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza alizofanya, wakasikiliza kwa makini yale aliyosema. Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele, na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo. Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu, nao watu wote, wakubwa kwa wadogo, wakamsikiliza na kustaajabu, wakisema, “Mtu huyu ndiye ajulikanaye kama Uweza Mkuu wa Mungu.” Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake. Lakini watu walipomwamini Filipo akihubiri Habari Njema ya ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.