Matendo 7:9-16
Matendo 7:9-16 Biblia Habari Njema (BHN)
“Wale mababu walimwonea wivu Yosefu, wakamwuza utumwani Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye, akamwokoa katika taabu zake zote. Mungu alimjalia fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri, hata Farao akamweka awe mkuu wa ile nchi na nyumba ya kifalme. Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula chochote. Basi, Yakobo aliposikia habari kwamba huko Misri kulikuwa na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya kwanza. Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu. Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla watu sabini na watano, waje Misri. Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu wengine walikufa. Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alikuwa amenunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.
Matendo 7:9-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye, akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote. Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha. Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza. Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao. Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano. Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu; wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Abrahamu alilinunua kwa kima fulani cha fedha kutoka kwa wana wa Hamori, huko Shekemu.
Matendo 7:9-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. Mungu akawa pamoja naye, akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya Misri na nyumba yake yote. Basi kukawa njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, na dhiki nyingi, wala baba zetu hawakupata chakula cha kuwatosha. Hata Yakobo aliposikia ya kwamba huko Misri kuna nafaka, akawatuma baba zetu mara ya kwanza. Hata safari ya pili Yusufu akajitambulisha kwa ndugu zake, jamaa ya Yusufu ikawa dhahiri kwa Farao. Yusufu akatuma watu akamwita Yakobo babaye na jamaa zake wote pia, watu sabini na watano. Basi Yakobo akashuka mpaka Misri; akafa yeye na baba zetu; wakachukuliwa mpaka Shekemu wakazikwa katika kaburi lile, ambalo Ibrahimu alilinunua kwa kima cha fedha kwa wana wa Hamori, huko Shekemu.
Matendo 7:9-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Kwa sababu hao baba zetu wa zamani walimwonea wivu Yusufu ndugu yao, walimuuza kama mtumwa huko Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye. Akamwokoa kutoka mateso yote yaliyompata. Tena Mungu akampa Yusufu kibali na hekima aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Naye Farao akamweka kuwa mtawala wa Misri na wa jumba lote la kifalme. “Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa, nao baba zetu wakawa hawana chakula. Lakini Yakobo aliposikia kwamba kuna nafaka huko Misri, aliwatuma baba zetu, wakaenda huko kwa mara yao ya kwanza. Walipoenda mara ya pili, Yusufu alijitambulisha kwa ndugu zake; naye Farao akapata habari kuhusu ndugu za Yusufu. Ndipo Yusufu akawatuma kumleta Yakobo baba yake pamoja na jamaa yake yote; kwa jumla walikuwa watu sabini na watano. Hivyo Yakobo akaenda Misri ambako yeye na baba zetu walifia. Miili yao ilirudishwa Shekemu na kuzikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alinunua kutoka kwa wana wa Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.