Matendo 7:1-8
Matendo 7:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, kuhani mkuu akamwuliza, “Je, mambo haya ni kweli?” Naye Stefano akasema, “Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni! Mungu alimtokea babu yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia kabla hajaenda kukaa kule Harani. Mungu alimwambia: ‘Ondoka katika nchi yako; waache watu wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonesha!’ Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa. Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake; hata hivyo, alimwahidi kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje wakati huu hakuwa na mtoto. Mungu alimwambia hivi: ‘Wazawa wako watapelekwa katika nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa vibaya kwa muda wa miaka 400. Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.’ Halafu Mungu akafanya naye agano ambalo tohara ni ishara yake. Hivyo, Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka, vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na wawili vivyo hivyo.
Matendo 7:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo? Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani, akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonesha. Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa. Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto. Mungu akanena hivi, ya kwamba wazawa wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne. Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa. Akampa agano la tohara; basi Abrahamu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu.
Matendo 7:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kuhani Mkuu akasema, Je! Mambo hayo ndivyo yalivyo? Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani, akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonyesha. Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, akakaa Harani, akatoka huko baada ya kufa babaye, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa. Wala hakumpa urithi humu hata kiasi cha kuweka mguu; akaahidi kwamba atampa, iwe milki yake, na ya uzao wake baadaye alipokuwa hana mtoto. Mungu akanena hivi, ya kwamba wazao wake watakuwa wageni katika nchi ya watu wengine, nao watawafanya kuwa watumwa wao, na kuwatenda mabaya kwa muda wa miaka mia nne. Na lile taifa watakaowafanya watumwa nitawahukumu mimi, alisema Mungu; na baada ya hayo watatoka, nao wataniabudu mahali hapa. Akampa agano la tohara; basi Ibrahimu akamzaa Isaka, akamtahiri siku ya nane. Isaka akamzaa Yakobo. Yakobo akawazaa wale kumi na wawili, wazee wetu.
Matendo 7:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo kuhani mkuu akamuuliza Stefano, “Je, mashtaka haya ni ya kweli?” Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni! Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa bado yuko Mesopotamia, kabla hajaishi Harani, akamwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na katika jamii yako, uende hadi nchi nitakayokuonesha.’ “Hivyo aliondoka katika nchi ya Wakaldayo akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu akamtoa huko akamleta katika nchi hii ambayo mnaishi sasa. Mungu hakumpa urithi wowote katika nchi hii, hakumpa hata mahali pa kuweka wayo mmoja. Bali Mungu alimwahidi kuwa yeye na uzao wake baada yake wangeirithi hii nchi, ingawa wakati huo Abrahamu hakuwa na mtoto. Mungu akasema naye hivi: ‘Wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne.’ Mungu akasema, ‘Lakini mimi nitaliadhibu taifa watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka katika nchi hiyo na wataniabudu mahali hapa.’ Ndipo akampa Abrahamu agano la tohara. Naye Abrahamu akamzaa Isaka na kumtahiri siku ya nane. Baadaye Isaka akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale baba zetu wa zamani kumi na wawili.