Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 3:1-12

Matendo 3:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wakienda hekaluni, wakati wa sala. Wakati huo watu walikuwa wanambeba mtu mmoja kiwete tangu kuzaliwa. Watu hao walikuwa wakimweka huyo mtu kila siku kwenye mlango wa hekalu uitwao “Mlango Mzuri,” ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia hekaluni. Alipowaona Petro na Yohane wakiingia hekaluni, aliwaomba wampe chochote. Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, “Tutazame!” Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Kisha Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu. Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu. Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu. Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata. Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa, wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane. Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea?

Shirikisha
Soma Matendo 3

Matendo 3:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Siku moja, Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali, yapata saa tisa alasiri. Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni. Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka. Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.” Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nitakachokupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu. Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu, wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu kwa yale yaliyomtukia. Aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wakiwakimbilia pale Ukumbi wa Sulemani. Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi Waisraeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumemfanya mtu huyu kutembea?

Shirikisha
Soma Matendo 3