Matendo 27:13-44
Matendo 27:13-44 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, upepo mzuri wa kusi ulianza kuvuma, nao wakadhani wamefanikiwa lengo lao; hivyo wakangoa nanga, wakaiendesha meli karibu sana na pwani ya Krete. Lakini haukupita muda, upepo mkali uitwao “Upepo wa Kaskazi” ulianza kuvuma kutoka kisiwani. Upepo uliipiga ile meli, na kwa kuwa hatukuweza kuukabili, tukaiacha ikokotwe na huo upepo. Kisiwa kimoja kiitwacho Kauda kilitukinga kidogo na ule upepo; na tulipopita kusini mwake tulifaulu, ingawa kwa shida, kuusalimisha ule mtumbwi wa meli. Wale wanamaji waliuvuta mtumbwi ndani, kisha wakaizungushia meli kamba na kuifunga kwa nguvu. Waliogopa kwamba wangeweza kukwama kwenye ufuko wa bahari, pwani ya Libia. Kwa hiyo walishusha matanga na kuiacha meli ikokotwe na upepo. Dhoruba iliendelea kuvuma na kesho yake wakaanza kutupa nje shehena ya meli. Siku ya tatu, wakaanza pia kutupa majini vifaa vya meli kwa mikono yao wenyewe. Kwa muda wa siku nyingi hatukuweza kuona jua wala nyota; dhoruba iliendelea kuvuma sana, hata matumaini yote ya kuokoka yakatuishia. Baada ya kukaa muda mrefu bila kula chakula, Paulo alisimama kati yao, akasema, “Waheshimiwa, ingalikuwa afadhali kama mngalinisikiliza na kuacha kusafiri kutoka Krete. Kama mngalifanya hivyo tungaliiepuka shida hii na hasara hizi zote. Lakini sasa ninawaombeni muwe na moyo; hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake; meli tu ndiyo itakayopotea. Kwa maana jana usiku malaika wa yule Mungu ambaye mimi ni wake na ambaye mimi ninamwabudu alinitokea, akaniambia: ‘Paulo, usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri nawe wasiangamie.’ Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa. Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa fulani.” Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku na huko katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi kuwa karibu na nchi kavu. Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arubaini. Baadaye wakapima tena wakapata mita thelathini. Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba, waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi. Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa mbele wa meli. Lakini Paulo alimwambia yule ofisa wa jeshi na askari wake, “Kama wanamaji hawa hawabaki ndani ya meli, hamtaokoka.” Hapo wale askari walizikata kamba zilizokuwa zimeshikilia ule mtumbwi, wakauacha uchukuliwe na maji. Karibu na alfajiri, Paulo aliwahimiza wote wale chakula: “Kwa siku kumi na nne sasa mmekuwa katika mashaka na bila kula; hamjala kitu chochote. Basi, ninawasihi mle chakula kwa maana mnakihitaji ili mweze kuendelea kuishi. Maana hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea.” Baada ya kusema hivyo, Paulo alichukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega, akaanza kula. Hapo wote wakapata moyo, nao pia wakala chakula. Jumla tulikuwa watu 276 katika meli. Baada ya kila mmoja kula chakula cha kutosha, walipunguza uzito wa meli kwa kutupa nafaka baharini. Kulipokucha, wanamaji hawakuweza kuitambua nchi ile, ila waliona ghuba moja yenye ufuko; wakaamua kutia nanga huko kama ikiwezekana. Hivyo walikata nanga na kuziacha baharini, na wakati huohuo wakazifungua kamba zilizokuwa zimeufunga usukani, kisha wakatweka tanga moja mbele kushika upepo, wakaelekea ufukoni. Lakini walifika mahali ambapo mikondo miwili ya bahari hukutana, na meli ikakwama. Sehemu ya mbele ilikuwa imezama mchangani bila kutikisika. Sehemu ya nyuma ya meli ilianza kuvunjika vipandevipande kwa mapigo ya nguvu ya mawimbi. Askari walitaka kuwaua wafungwa wote kwa kuogopa kwamba wangeogelea hadi pwani na kutoroka. Lakini kwa vile yule ofisajeshi alitaka kumwokoa Paulo, aliwazuia wasifanye hivyo. Aliamuru wale waliojua kuogelea waruke kutoka melini na kuogelea hadi pwani, na wengine wafuate wakijishikilia kwenye mbao au kwenye vipande vya meli iliyovunjika. Ndivyo sisi sote tulivyofika salama pwani.
Matendo 27:13-44 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang'oa nanga, wakasafiri karibu na Krete kandokando ya pwani. Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo, merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa. Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida. Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi. Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, kesho yake wakaanza kuitupa shehena baharini. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa. Lakini hatuna budi kupwelewa katika kisiwa kimoja. Hata usiku wa kumi na nne ulipofika, tulipokuwa tukichukuliwa huku na huko katika bahari ya Adria, kama usiku wa manane baharia wakadhani ya kuwa wanaikaribia nchi kavu. Wakatupa bildi wakapata pima ishirini, wakaendelea kidogo wakatupa bildi tena, wakapata pima kumi na tano. Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche. Na baharia walipotaka kukimbia na kuiacha merikebu, wakiishusha mashua baharini kana kwamba wanataka kutupa nanga za omo, Paulo akawaambia ofisa na askari, Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka. Basi askari wakazikata kamba za mashua, wakaiacha ianguke. Na kulipokuwa kukipambazuka Paulo akawasihi wote wale chakula, akisema, Leo ni siku ya kumi na nne kungoja na kufunga, hamkula kitu chochote. Basi nawasihi mle chakula, maana itakuwa kwa wokovu wenu; kwa maana hapana hata unywele wa kichwa cha mmoja wenu utakaopotea. Alipokwisha kusema hayo akatwaa mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega akaanza kula. Ndipo wakachangamka wote, wakala chakula wenyewe. Na sisi tuliokuwa ndani ya merikebu tulikuwa watu mia mbili na sabini na sita. Walipokwisha kushiba wakaipunguza shehena ya merikebu, wakiitupa ngano baharini. Kulipokucha hawakuitambua ile nchi, ila waliona hori yenye ufuo, wakashauriana kuiegesha merikebu huko, kama ikiwezekana. Wakazitupilia mbali zile nanga, na kuziacha baharini, pamoja na kuzilegeza kamba za sukani, wakalitweka tanga dogo ili liushike upepo, wakauendea ule ufuo. Lakini wakafikia mahali palipokutana bahari mbili, wakaiegesha merikebu, omo ikakwama ikakaa isitikiswe, bali tezi ilikuwa imefumuliwa kwa nguvu za mawimbi. Mpango wa askari ulikuwa kuwaua wafungwa, mtu asiogelee na kukimbia. Bali ofisa, akitaka kumponya Paulo, akawazuia, wasifanye kama walivyokusudia, akawaamuru wale wawezao kuogelea wajitupe kwanza baharini, wafike katika nchi kavu; nao waliosalia, hawa juu ya mbao na hawa juu ya vitu vingine vya merikebu. Na hivyo watu wote wakapata kuifikia nchi kavu salama.
Matendo 27:13-44 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang’oa nanga, wakasafiri karibu na Krete pwani kwa pwani. Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo, merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa. Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida. Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi. Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa shehena baharini. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung’oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa. Lakini hatuna budi kupwelewa katika kisiwa kimoja. Hata usiku wa kumi na nne ulipofika, tulipokuwa tukichukuliwa huko na huko katika bahari ya Adria, kama usiku wa manane baharia wakadhani ya kuwa wanaikaribia nchi kavu. Wakatupa bildi wakapata pima ishirini, wakaendelea kidogo wakatupa bildi tena, wakapata pima kumi na tano. Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche. Na baharia walipotaka kukimbia na kuiacha merikebu, wakiishusha mashua baharini kana kwamba wanataka kutupa nanga za omo, Paulo akawaambia akida na askari, Hawa wasipokaa ndani ya merikebu hamtaweza kuokoka. Basi askari wakazikata kamba za mashua, wakaiacha ianguke. Na kulipokuwa kukipambauka Paulo akawasihi wote wale chakula, akisema, Leo ni siku ya kumi na nne kungoja na kufunga, hamkula kitu cho chote. Basi nawasihi mle chakula, maana itakuwa kwa wokovu wenu; kwa maana hapana hata unywele wa kichwa cha mmoja wenu utakaopotea. Alipokwisha kusema hayo akatwaa mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote akaumega akaanza kula. Ndipo wakachangamka wote, wakala chakula wenyewe. Na sisi tuliokuwa ndani ya merikebu tulipata watu mia mbili na sabini na sita. Walipokwisha kushiba wakaipunguza shehena ya merikebu, wakiitupa ngano baharini. Kulipokucha hawakuitambua ile nchi, ila waliona hori yenye ufuo, wakashauriana kuiegesha merikebu huko, kama ikiwezekana. Wakazitupilia mbali zile nanga, na kuziacha baharini, pamoja na kuzilegeza kamba za sukani, wakalitweka tanga dogo ili liushike upepo, wakauendea ule ufuo. Lakini wakafikia mahali palipokutana bahari mbili, wakaiegesha merikebu, omo ikakwama ikakaa isitikiswe, bali tezi ilikuwa imefumuliwa kwa nguvu za mawimbi. Shauri la askari lilikuwa kuwaua wafungwa, mtu asiogelee na kukimbia. Bali akida, akitaka kumponya Paulo, akawazuia, wasifanye kama walivyokusudia, akawaamuru wale wawezao kuogelea wajitupe kwanza baharini, wafike nchi kavu; nao waliosalia, hawa juu ya mbao na hawa juu ya vitu vingine vya merikebu. Na hivyo watu wote wakapata kuifikilia nchi kavu salama.
Matendo 27:13-44 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Upepo mtulivu ulipoanza kuvuma toka kusini, wakadhani kuwa wangeweza kufikia lengo lao, hivyo wakangʼoa nanga na kusafiri wakipita kandokando ya pwani ya kisiwa cha Krete. Lakini baada ya muda mfupi, ikavuma tufani kubwa iitwayo Eurakilo kutoka kisiwa cha Krete. Meli ikapigwa na dhoruba na haikuweza kushindana na ule upepo, tukarudishwa baharini upepo ulikokuwa unaelekea. Hatimaye tukisafiri kupita chini ya kisiwa kidogo kiitwacho Kauda, ambapo kwa kuwa tulikuwa tumekingiwa upepo na hicho kisiwa, tuliweza kwa shida kuifunga mashua ya kuokolea watu. Watu walipokwisha kuivuta mashua hiyo na kuiingiza katika meli, waliifunga kwa kamba chini ya meli yenyewe ili kuzishikanisha pamoja. Wakiogopa kupelekwa kwenye mchanga karibu na pwani ya Sirti, wakashusha matanga wakaiacha meli isukumwe na huo upepo. Tulikuwa tunapigwa na dhoruba kwa nguvu, kiasi kwamba kesho yake walianza kutupa shehena toka kwenye meli. Siku ya tatu, wakatupa vyombo vya meli baharini kwa mikono yao wenyewe. Wakati jua wala nyota hazikuonekana kwa siku nyingi, na dhoruba iliendelea kuvuma, hatimaye tulikata tamaa ya kuokolewa. Baada ya watu kukaa siku nyingi bila kula chakula, Paulo akasimama mbele yao na kusema: “Enyi watu, kama mngekubali ushauri wangu wa kutosafiri kwa meli kutoka Krete, basi mngejiepusha na uharibifu na hasara hii. Sasa ninawasihi sana, jipeni moyo kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake, ila meli itaangamia. Jana usiku, malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake na ninayemwabudu alisimama karibu nami, akaniambia, ‘Paulo usiogope, kwa kuwa ni lazima usimame mbele ya Kaisari, naye Mungu amekupa kwa neema uhai wa wote wanaosafiri pamoja nawe.’ Hivyo jipeni moyo, enyi watu, kwa kuwa ninamwamini Mungu kwamba yatakuwa kama vile alivyoniambia. Lakini hata hivyo meli yetu itakwama kwenye kisiwa fulani.” Usiku wa kumi na nne ulipofika, tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika Bahari ya Adria. Ilipokuwa yapata usiku wa manane, mabaharia wakahisi kwamba walikuwa wanakaribia nchi kavu. Kwa hiyo wakapima kina cha maji na kukuta kilikuwa pima ishirini; baada ya kuendelea mbele kidogo, wakapima tena wakapata kina cha pima kumi na tano. Wakiogopa kwamba meli yetu ingegonga kwenye miamba, wakashusha nanga nne za nyuma ya meli, wakawa wanaomba kupambazuke. Katika jaribio la kutoroka kutoka kwa meli, mabaharia wakashusha mashua ya kuokolea watu baharini, wakijifanya kwamba wanaenda kushusha nanga za omo. Ndipo Paulo akamwambia yule jemadari na askari, “Hawa watu wasipobaki katika meli, hamtaweza kuokoka.” Hivyo basi wale askari wakakata kamba zilizoshikilia ile mashua ya kuokolea watu kwenye meli, wakaiacha ianguke humo baharini. Kabla ya mapambazuko, Paulo akawasihi watu wote wale chakula akisema, “Leo ni siku ya kumi na nne mmekuwa katika wasiwasi mkiwa mmefunga na bila kula chochote. Kwa hiyo nawasihi mle chakula, kwa maana itawasaidia ili mweze kuishi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza unywele hata mmoja kutoka kichwani mwake.” Baada ya kusema maneno haya, Paulo akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega akaanza kula. Ndipo wote wakatiwa moyo, wakaanza kula chakula. Ndani ya meli tulikuwa jumla ya watu mia mbili na sabini na sita (276). Baada ya watu wote kula chakula cha kutosha, wakapunguza uzito wa meli kwa kutupa ngano baharini. Kulipopambazuka, mabaharia hawakuitambua ile nchi, lakini waliona ghuba yenye ufuko wa mchanga, ambako waliamua kuipweleza meli kama ingewezekana. Kwa hiyo wakatupa nanga zote na kuziacha baharini, na wakati huo huo wakalegeza kamba zilizokuwa zikishikilia usukani wa meli. Kisha wakatweka tanga la mbele lishike upepo na kuisukuma meli kuelekea pwani. Lakini wakafika mahali bahari mbili zinakutana, wakaipweleza meli ufuoni; omo ikakwama sana, ikawa haiwezi kuondolewa; lakini sehemu ya shetri ikavunjika vipande vipande kutokana na kupigwa kwa mawimbi yenye nguvu. Wale askari wakapanga kuwaua wale wafungwa ili kuzuia hata mmoja wao asiogelee na kutoroka. Lakini yule jemadari alitaka kuokoa maisha ya Paulo, basi akawazuia askari wasitekeleze mpango wao. Akaamuru wale wanaoweza kuogelea wajitupe baharini kwanza, waogelee hadi nchi kavu. Waliosalia wangefika nchi kavu kwa kutumia mbao au vipande vya meli iliyovunjika, hivyo wote wakafika nchi kavu salama.