Matendo 25:13-19
Matendo 25:13-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku chache baadaye, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisarea ili kutoa heshima zao kwa Festo. Walikuwa huko siku kadhaa naye Festo akamweleza mfalme kesi ya Paulo: “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Felisi alimwacha kizuizini. Nilipokwenda Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walimshtaki na kuniomba nimhukumu. Lakini mimi niliwajibu kwamba si desturi ya Waroma kumtoa mtu aadhibiwe kabla mshtakiwa hajakutana na washtaki wake ana kwa ana na kupewa fursa ya kujitetea kuhusu hayo mashtaka. Basi, walipofika hapa sikukawia, ila nilifanya kikao mahakamani kesho yake, nikaamuru mtu huyo aletwe. Washtaki wake walisimama lakini hawakutoa mashtaka maovu kama nilivyokuwa ninatazamia. Ila tu walikuwa na mabishano kadhaa pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu mmoja aitwaye Yesu ambaye alikufa, lakini Paulo anashikilia kwamba yu hai.
Matendo 25:13-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku kadhaa zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokaa huko siku kadhaa, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lolote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali tofauti tofauti juu yake katika dini yao wenyewe, na kuhusu mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikazania kusema kuwa yuko hai.
Matendo 25:13-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku kadha wa kadha zilipokwisha kupita, Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai.
Matendo 25:13-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo. Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili kesi ya Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani. Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake. “Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu yeyote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa. Hivyo walipokutana hapa, sikukawia, kesho yake niliitisha baraza, nikaketi kwenye kiti changu cha hukumu, nikaagiza huyo mtu aletwe. Washtaki wake walipoinuka kuzungumza, hawakumshtaki kwa uhalifu wowote kama nilivyotarajia. Badala yake walikuwa na vipengele fulani vya kutokukubaliana naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu aitwaye Yesu aliyekufa, lakini Paulo alidai kwamba yu hai.