Matendo 22:6-21
Matendo 22:6-21 Biblia Habari Njema (BHN)
“Basi, nilipokuwa njiani karibu na kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwanga mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote. Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?’ Nami nikauliza, ‘Nani wewe, Bwana?’ Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.’ Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami. Basi, mimi nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’ Naye Bwana akaniambia, ‘Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.’ Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko. “Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko. Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Saulo! Ona tena.’ Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia. Halafu Anania akasema, ‘Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea. Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia. Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama, ubatizwe na kuondolewa dhambi zako kwa kuliungama jina lake.’ “Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali hekaluni, niliona maono. Nilimwona Bwana akiniambia, ‘Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.’ Nami nikamjibu, ‘Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini. Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.’ Naye Bwana akaniambia, ‘Nenda; nitakutuma mbali kwa mataifa mengine.’”
Matendo 22:6-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafla nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski. Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko, Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, pata kuona tena. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa, mbona unakawia? Simama, ubatizwe, ukaoshwe dhambi zako, ukiliitia jina lake. Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa katika hali ya kuzimia roho, nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako kuhusu habari zangu. Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nilikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi. Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua. Naye akaniambia, Nenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.
Matendo 22:6-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski. Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko, Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake. Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho, nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu. Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi. Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua. Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.
Matendo 22:6-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Nilipokuwa njiani kuelekea Dameski, yapata saa sita mchana, ghafula nuru kubwa kutoka mbinguni ikanimulika kotekote. Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli! Sauli! Mbona unanitesa?’ “Nikajibu, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ “Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti unayemtesa.’ Basi wale watu waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia sauti ya yule aliyekuwa akisema nami. “Nikauliza, ‘Nifanye nini, Bwana?’ “Naye Bwana akaniambia, ‘Inuka uingie Dameski, huko utaambiwa yote unayopaswa kufanya.’ Kwa kuwa nilikuwa siwezi kuona kwa ajili ya mngʼao wa ile nuru, wenzangu wakanishika mkono wakaniongoza kuingia Dameski. “Mtu mmoja mcha Mungu, jina lake Anania, alikuja kuniona. Alizishika sana sheria zetu, na aliheshimiwa sana na Wayahudi walioishi huko Dameski. Akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Sauli, pata kuona tena!’ Nami mara hiyo nikaweza kumwona. “Akasema, ‘Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe ili ujue mapenzi yake, umwone yeye Aliye Mwenye Haki na upate kusikia maneno kutoka kinywani mwake. Kwa kuwa utakuwa shahidi wake kwa watu kuhusu kile ulichokiona na kukisikia. Sasa basi, mbona unakawia? Inuka, ukabatizwe na dhambi zako zikasafishwe, ukiliita Jina lake.’ “Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula, nikamwona Bwana akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu.’ “Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyoenda kwenye kila sinagogi ili kuwatupa gerezani na kuwapiga wale waliokuamini. Damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomuua.’ “Ndipo Bwana akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’ ”