Matendo 21:1-9
Matendo 21:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Tulipokwisha agana nao, tulipanda meli tukaenda moja kwa moja mpaka Kosi. Kesho yake tulifika Rode, na kutoka huko tulikwenda Patara. Huko, tulikuta meli iliyokuwa inakwenda Foinike, hivyo tulipanda, tukasafiri. Baada ya kufika mahali ambapo tuliweza kuona Kupro, tulipitia upande wake wa kusini tukaelekea Siria. Tulitia nanga katika mji wa Tiro ambapo ile meli ilikuwa ipakuliwe shehena yake. Tulikuta waumini huko, tukakaa pamoja nao kwa muda wa juma moja. Waumini hao wakawa wanaongea kwa nguvu ya Roho, wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu. Lakini muda wetu ulipokwisha tuliondoka. Wote pamoja na wanawake na watoto wao walitusindikiza mpaka nje ya mji. Tulipofika pwani, sote tulipiga magoti tukasali. Kisha tuliagana; sisi tukapanda meli, nao wakarudi makwao. Sisi tuliendelea na safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai ambapo tuliwasalimu ndugu zetu, tukakaa nao siku moja. Kesho yake tuliondoka tukaenda Kaisarea. Huko tulikwenda nyumbani kwa mhubiri Filipo. Yeye alikuwa mmoja wa wale saba waliochaguliwa kule Yerusalemu. Alikuwa na binti wanne ambao walikuwa na kipaji cha unabii.
Matendo 21:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa tulipokwisha kujitenga nao na kuabiri, tukafika Kosi kwa tanga moja, na kesho yake tukafika Rodo na kutoka huko tukafika Patara, tukapata merikebu itakayovuka mpaka Foinike tukapanda tukatweka. Na tulipoona Kipro tukaiacha upande wa kushoto; tukasafiri mpaka Shamu tukashuka Tiro. Kwa maana huko ndiko merikebu yetu itakakoshusha shehena yake. Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho asipande kwenda Yerusalemu. Hata tulipotimiza siku zile tukaondoka tukaenda zetu, na watu wote, pamoja na wake zao na watoto wao, wakatusindikiza mpake nje ya mji, tukapiga magoti pwani tukaomba; na baada ya kuagana tukapanda melini, nao wakarudi kwao. Tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja. Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake. Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri.
Matendo 21:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa tulipokwisha kujitenga nao na kuabiri, tukafika Kosi kwa tanga moja, na siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukafika Patara, tukapata merikebu itakayovuka mpaka Foinike tukapanda tukatweka. Na tulipoona Kipro tukaiacha upande wa kushoto; tukasafiri mpaka Shamu tukashuka Tiro. Kwa maana huko ndiko merikebu yetu itakakoshusha shehena yake. Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho asipande kwenda Yerusalemu. Hata tulipotimiza siku zile tukaondoka tukaenda zetu, na watu wote, pamoja na wake zao na watoto wao, wakatusindikiza mpake nje ya mji, tukapiga magoti pwani tukaomba; na baada ya kuagana tukapanda merikebuni, nao wakarudi kwao. Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja. Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake. Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri.
Matendo 21:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Tulipokwisha kujitenga nao, tukasafiri kwa meli moja kwa moja hadi Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo, na kutoka huko tukaenda Patara. Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo. Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri hadi Siria. Tukatia nanga katika bandari ya Tiro, ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake. Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu. Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba. Baada ya kuagana, tukapanda kwenye meli, nao wakarudi manyumbani mwao. Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu ndugu wa huko, tukakaa nao kwa siku moja. Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani mwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake. Filipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.