Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 20:13-38

Matendo 20:13-38 Biblia Habari Njema (BHN)

Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu. Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene. Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto. Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana. Kutoka Mileto Paulo alituma ujumbe kwa wazee wa Efeso wakutane naye. Walipofika kwake aliwaambia, “Mnajua jinsi nilivyokaa nanyi siku zote tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia. Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi. Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni. Niliwaonya wote – Wayahudi, kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu. Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko. Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea. Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa kitu sana kwangu mradi tu nikamilishe ule utume wangu na ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nishuhudie Habari Njema ya neema ya Mungu. “Nimepita miongoni mwenu nyote nikiuhubiri ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu atakayeniona tena. Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote. Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio lote la Mungu. Jihadharini wenyewe; lilindeni lile kundi ambalo Roho Mtakatifu amewaweka nyinyi muwe walezi wake. Lichungeni kanisa la Mungu ambalo amejipatia kwa damu ya Mwanae. Nafahamu vizuri sana kwamba baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali watawavamieni, na hawatakuwa na huruma kwa kundi hilo. Hata kutoka miongoni mwenu watatokea watu ambao watasema mambo ya uongo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate wao tu. Kwa hiyo, muwe macho mkikumbuka kwamba kwa muda wa miaka mitatu, usiku na mchana, sikuchoka kumwonya kila mmoja wenu kwa machozi. “Na sasa basi, ninawaweka nyinyi chini ya ulinzi wa Mungu na ujumbe wa neema yake. Yeye anao uwezo wa kuwajenga na kuwawezesha mzipate zile baraka alizowawekea watu wake. Mimi sikutamani hata mara moja fedha, wala dhahabu, wala nguo za mtu yeyote. Mnajua nyinyi wenyewe kwamba nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe, ili kujipatia mahitaji yangu na ya wenzangu. Nimekuwa nikiwapeni daima mfano kwamba kwa kufanya kazi mithili hiyo tunapaswa kuwasaidia walio dhaifu, tukikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe: ‘Heri zaidi kutoa kuliko kupokea.’” Baada ya kusema hayo, Paulo alipiga magoti pamoja nao wote, akasali. Wote walikuwa wanalia, na kumwaga kwa kumkumbatia na kumbusu. Jambo lililowahuzunisha zaidi lilikuwa neno alilosema kwamba hawangemwona tena. Basi, wakamsindikiza hadi melini.

Shirikisha
Soma Matendo 20

Matendo 20:13-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimia kwenda kwa miguu. Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene. Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto. Kwa sababu Paulo alikusudia kusafiri pasipo kupitia Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana. Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kutokana na njama za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lolote liwezalo kuwafaa bali niliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wagiriki wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu nikiwa nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu. Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huku na huko, hamtaniona uso tena. Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote. Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu. Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawafuatie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusubusu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

Shirikisha
Soma Matendo 20

Matendo 20:13-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimu kwenda kwa miguu. Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene. Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto. Kwa sababu Paulo amekusudia kupita Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana. Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu. Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena. Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote. Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu. Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

Shirikisha
Soma Matendo 20

Matendo 20:13-38 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Tukatangulia kwenye meli, tukasafiri kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Alikuwa amefanya utaratibu huu kwa sababu alikuwa akienda huko kwa miguu. Alipotukuta huko Aso, alijiunga nasi kwenye meli, tukasafiri hadi Mitilene. Kutoka huko tuliendelea kwa meli, na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo, na kesho yake tukawasili Mileto. Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko jimbo la Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste kama ingewezekana. Paulo akiwa Mileto, alituma mjumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa waje wakutane naye. Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi muda wote nilikuwa nanyi, tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa jimbo la Asia. Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo. “Nami sasa nimesukumwa na Roho, ninaenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko. Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja. Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Yesu aliyonipa, yaani kazi ya kuishuhudia Injili ya neema ya Mungu. “Nami sasa najua kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu niliowahubiria ufalme wa Mungu atakayeniona tena. Kwa hiyo nawatangazia leo, sina hatia ya damu ya mtu yeyote. Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu. Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua kwamba baada yangu kuondoka, mbwa-mwitu wakali watakuja kati yenu, ambao hawatalihurumia kundi. Hata kutoka miongoni mwenu watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya kila mmoja kwa machozi usiku na mchana. “Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu wala vazi la mtu yeyote. Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika kila jambo nimewaonesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ” Paulo alipomaliza kusema haya akapiga magoti pamoja nao wote akaomba. Wote wakalia, wakamkumbatia Paulo na kumbusu. Kilichowahuzunisha zaidi ni kwa sababu ya yale maneno aliyosema kwamba kamwe hawatauona uso wake tena. Wakaenda naye hadi kwenye meli.

Shirikisha
Soma Matendo 20