Matendo 20:1-6
Matendo 20:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Ile ghasia ya Efeso ilipokwisha tulia Paulo aliwaita pamoja wale waumini, akawatia moyo. Kisha akawaaga, akasafiri kwenda Makedonia. Alipitia sehemu za nchi zile akiwatia watu moyo kwa maneno mengi. Halafu akafika Ugiriki ambako alikaa kwa miezi mitatu. Alipokuwa anajitayarisha kwenda Siria, aligundua kwamba Wayahudi walikuwa wanamfanyia mpango mbaya; hivyo aliamua kurudi kwa kupitia Makedonia. Sopatro, mwana wa Pirho, kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia. Hao walitutangulia na kutungojea kule Troa. Sisi, baada ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja.
Matendo 20:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ghasia ile ilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia. Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Ugiriki. Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia. Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberea, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia. Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa. Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, baada ya safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba.
Matendo 20:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kishindo kile kilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia. Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Uyunani. Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia. Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberoya, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia. Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa. Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba.
Matendo 20:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya zile ghasia kumalizika, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia. Alipita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo. Ndipo hatimaye akawasili Uyunani, ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Kwa sababu baadhi ya Wayahudi walikuwa wamepanga njama dhidi yake alipokuwa karibu kusafiri kwa meli kwenda Siria, aliamua kurudi kupitia Makedonia. Paulo aliandamana na Sopatro mwana wa Piro kutoka Beroya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, na Gayo kutoka Derbe, pia Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka jimbo la Asia. Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa. Lakini sisi tukasafiri kwa meli kwa siku tano kutoka Filipi baada ya siku za Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, nasi tukaungana na wengine huko Troa, ambako tulikaa kwa siku saba.