Matendo 20:1-16
Matendo 20:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Ile ghasia ya Efeso ilipokwisha tulia Paulo aliwaita pamoja wale waumini, akawatia moyo. Kisha akawaaga, akasafiri kwenda Makedonia. Alipitia sehemu za nchi zile akiwatia watu moyo kwa maneno mengi. Halafu akafika Ugiriki ambako alikaa kwa miezi mitatu. Alipokuwa anajitayarisha kwenda Siria, aligundua kwamba Wayahudi walikuwa wanamfanyia mpango mbaya; hivyo aliamua kurudi kwa kupitia Makedonia. Sopatro, mwana wa Pirho, kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia. Hao walitutangulia na kutungojea kule Troa. Sisi, baada ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja. Jumamosi jioni tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane. Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka. Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa. Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, “Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake.” Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka. Wale watu walimchukua yule kijana hadi nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa. Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu. Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene. Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto. Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana.
Matendo 20:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ghasia ile ilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia. Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Ugiriki. Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia. Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberea, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia. Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa. Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, baada ya safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba. Siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubia, maana aliazimia kusafiri siku iliyofuata, naye akafululiza maneno yake hadi usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika ghorofa lile tulipokuwa tumekusanyika. Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka ghorofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake. Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hadi alfajiri, ndipo akaenda zake. Wakamleta yule kijana, akiwa mzima, wakafarijika faraja kubwa sana. Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimia kwenda kwa miguu. Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene. Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto. Kwa sababu Paulo alikusudia kusafiri pasipo kupitia Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana.
Matendo 20:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kishindo kile kilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia. Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Uyunani. Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia. Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberoya, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia. Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa. Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba. Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika. Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake. Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake. Wakamleta yule kijana, yu mzima, wakafarijika faraja kubwa sana. Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimu kwenda kwa miguu. Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene. Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto. Kwa sababu Paulo amekusudia kupita Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana.
Matendo 20:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya zile ghasia kumalizika, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia. Alipita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo. Ndipo hatimaye akawasili Uyunani, ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Kwa sababu baadhi ya Wayahudi walikuwa wamepanga njama dhidi yake alipokuwa karibu kusafiri kwa meli kwenda Siria, aliamua kurudi kupitia Makedonia. Paulo aliandamana na Sopatro mwana wa Piro kutoka Beroya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, na Gayo kutoka Derbe, pia Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka jimbo la Asia. Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa. Lakini sisi tukasafiri kwa meli kwa siku tano kutoka Filipi baada ya siku za Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, nasi tukaungana na wengine huko Troa, ambako tulikaa kwa siku saba. Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea hadi usiku wa manane. Kwenye chumba cha ghorofani walimokuwa wamekutania kulikuwa na taa nyingi. Kijana mmoja jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akihubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamchukua akiwa amekufa. Paulo akashuka chini, akajitupa juu yake na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, bado yuko hai!” Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea hadi mapambazuko, akaondoka. Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana. Tukatangulia kwenye meli, tukasafiri kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Alikuwa amefanya utaratibu huu kwa sababu alikuwa akienda huko kwa miguu. Alipotukuta huko Aso, alijiunga nasi kwenye meli, tukasafiri hadi Mitilene. Kutoka huko tuliendelea kwa meli, na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo, na kesho yake tukawasili Mileto. Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko jimbo la Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste kama ingewezekana.