Matendo 2:14-24
Matendo 2:14-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi? Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli: ‘Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu wa kiume na wa kike watatoa unabii, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Naam, hata watumishi wangu wa kiume na kike, nitawamiminia Roho wangu siku zile, nao watatoa unabii. Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito; jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana. Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.’ “Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua. Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge.
Matendo 2:14-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Yudea, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi. Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri. Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa. Enyi wanaume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulubisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao.
Matendo 2:14-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi. Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri. Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa. Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao.
Matendo 2:14-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akapaza sauti yake na kuhutubia umati ule wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na nyote mnaoishi Yerusalemu, nisikilizeni kwa makini, ili jambo hili lijulikane kwenu. Hakika watu hawa hawajalewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema: “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu, nao watatabiri. Nami nitaonesha maajabu juu mbinguni, na ishara chini duniani: damu, moto, na mawimbi ya moshi. Jua litakuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana iliyo tukufu. Na kila mtu atakayeliitia jina la Bwana, ataokolewa.’ “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. Baada ya huyu mtu kutolewa kwenu kwa mpango wa Mungu uliokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi mlimuua kwa kumsulubisha msalabani, kwa mikono ya watu waovu. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.