Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 2:1-24

Matendo 2:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika mahali pamoja. Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikaijaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa. Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha. Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani. Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Walistaajabu na kushangaa wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya? Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe? Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelamu; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia, Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libia karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma, Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu.” Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana gani?” Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai mpya!” Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu. Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi? Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli: ‘Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu wa kiume na wa kike watatoa unabii, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Naam, hata watumishi wangu wa kiume na kike, nitawamiminia Roho wangu siku zile, nao watatoa unabii. Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito; jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana. Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.’ “Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua. Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge.

Shirikisha
Soma Matendo 2

Matendo 2:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakati ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafla toka mbinguni sauti kama mvumo wa upepo mkali ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Yudea na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya? Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya. Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Yudea, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi. Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri. Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa. Enyi wanaume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulubisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao.

Shirikisha
Soma Matendo 2

Matendo 2:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu. Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya? Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya. Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi. Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri. Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa. Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akiufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao.

Shirikisha
Soma Matendo 2

Matendo 2:1-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Siku ya Pentekoste ilipowadia, waumini wote walikuwa mahali pamoja. Ghafula, sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali ikatoka mbinguni, ikaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia. Basi walikuwako Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. Waliposikia sauti hii, umati wa watu walikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakiwa wameshangaa na kustaajabu, wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya? Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa? Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na jimbo la Asia, Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni kutoka Rumi (Wayahudi na wale walioongokea dini ya Kiyahudi), Wakrete na Waarabu: sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.” Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?” Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa kwa divai!” Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akapaza sauti yake na kuhutubia umati ule wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na nyote mnaoishi Yerusalemu, nisikilizeni kwa makini, ili jambo hili lijulikane kwenu. Hakika watu hawa hawajalewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema: “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu, nao watatabiri. Nami nitaonesha maajabu juu mbinguni, na ishara chini duniani: damu, moto, na mawimbi ya moshi. Jua litakuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana iliyo tukufu. Na kila mtu atakayeliitia jina la Bwana, ataokolewa.’ “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. Baada ya huyu mtu kutolewa kwenu kwa mpango wa Mungu uliokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi mlimuua kwa kumsulubisha msalabani, kwa mikono ya watu waovu. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.

Shirikisha
Soma Matendo 2