Matendo 19:1-16
Matendo 19:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati Apolo alipokuwa Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso ambako aliwakuta wanafunzi kadhaa. Akauliza, “Je, mlipopata kuwa waumini mlipokea Roho Mtakatifu?” Nao wakamjibu, “La! Hata hatujasikia kwamba kuna Roho Mtakatifu.” Naye akasema, “Sasa mlipata ubatizo wa namna gani?” Wakamjibu, “Ubatizo wa Yohane.” Naye Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa kuonesha kwamba watu wametubu. Yohane aliwaambia watu wamwamini yule ambaye alikuwa anakuja baada yake, yaani Yesu.” Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Basi, Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kusema lugha ngeni na kutangaza ujumbe wa Mungu. Wote jumla walikuwa watu wapatao kumi na wawili. Kwa muda wa miezi mitatu Paulo alikuwa akienda katika sunagogi, akawa na majadiliano ya kuvutia sana juu ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikuwa wakaidi, wakakataa kuamini, wakaanza kuongea vibaya juu ya hiyo njia ya Bwana katika kusanyiko la watu. Hapo Paulo alivunja uhusiano nao, akawachukua pembeni wale wanafunzi wake, akawa anazungumza nao kila siku katika jumba la masomo la Turano. Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana. Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo. Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao. Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya walisafiri huko na huko wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: “Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri.” Watoto saba wa Skewa, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo. Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini nyinyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.
Matendo 19:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadhaa huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na idadi yao ilikuwa kama wanaume kumi na wawili. Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa la mtu mmoja, jina lake Tirano. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wagiriki. Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawatoka, pepo wachafu wakawatoka. Baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwapo wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile wakiwa uchi na kujeruhiwa.
Matendo 19:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili. Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano. Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wayunani. Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka. Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.
Matendo 19:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa, akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?” Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.” Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.” Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani Yesu.” Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri. Walikuwa wapatao wanaume kumi na wawili. Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao wakakaidi; walikataa kuamini, na wakakashifu Njia Ile hadharani. Basi Paulo aliachana nao. Akaenda na wanafunzi wale, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano. Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko jimbo la Asia wakawa wamesikia neno la Bwana. Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kupitia kwa Paulo, hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka. Baadhi ya Wayahudi waliotangatanga wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu kwa wale wenye pepo, wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.” Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo. Siku moja pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?” Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.