Matendo 16:1-10
Matendo 16:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki. Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio. Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki. Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie. Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku. Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia. Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa. Usiku huo, Paulo aliona maono ambayo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: “Vuka, uje Makedonia ukatusaidie.” Mara baada ya Paulo kuona maono hayo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwahubirie Habari Njema.
Matendo 16:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Mgiriki. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Mgiriki. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike. Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakateremka kwenda Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubirie Habari Njema.
Matendo 16:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani. Mtu huyo alishuhudiwa vema na ndugu waliokaa Listra na Ikonio. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike. Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie. Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema.
Matendo 16:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani. Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio Paulo alitaka Timotheo aandamane naye, hivyo akamtahiri kwa sababu ya Wayahudi walioishi eneo lile, kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani. Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate. Hivyo makanisa yakaimarika katika imani, na kuongezeka kwa idadi kila siku. Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko jimbo la Asia. Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa. Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.” Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri Habari Njema huko.