Matendo 14:1-7
Matendo 14:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kule Ikonio, mambo yalikuwa kama yalivyokuwa kule Antiokia; Paulo na Barnaba walikwenda katika sunagogi la Wayahudi wakaongea kwa uhodari hata Wayahudi wengi na Wagiriki wakawa waumini. Lakini Wayahudi wengine waliokataa kuwa waumini walichochea na kutia chuki katika mioyo ya watu wa mataifa mengine ili wawapinge hao ndugu. Paulo na Barnaba waliendelea kukaa huko kwa muda mrefu. Waliongea kwa uhodari juu ya Bwana, naye Bwana akathibitisha ukweli wa ujumbe walioutoa juu ya neema yake, kwa kuwawezesha kutenda miujiza na maajabu. Watu wa mji huo waligawanyika: Wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa upande wa mitume. Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe. Mitume walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na katika sehemu za jirani, wakawa wanahubiri Habari Njema huko.
Matendo 14:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa huko Ikonio wakaingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi; na kwa vile walivyonena, kundi kubwa la Wayahudi na la Wagiriki wakaamini. Lakini Wayahudi wasioamini wakawataharakisha watu wa Mataifa na kuwatia nia mbaya juu ya ndugu. Basi wakakaa huko wakati mwingi, wakinena kwa ushujaa katika Bwana, aliyelishuhudia neno la neema yake, akiwajalia ishara na maajabu yatendeke kwa mikono yao. Lakini jamii ya watu wa mjini wakafarakana; hawa walikuwa upande wa Wayahudi, na hawa upande wa mitume. Hata palipotokea shambulio la watu wa Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao, kuwatenda jeuri na kuwapiga kwa mawe, wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia, na nchi zilizo kandokando; wakakaa huko, wakiihubiri Injili.
Matendo 14:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa huko Ikonio wakaingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi; na kwa vile walivyonena, kundi kubwa la Wayahudi na la Wayunani wakaamini. Walakini Wayahudi wasioamini wakawataharakisha watu wa Mataifa na kuwatia nia mbaya juu ya ndugu. Basi wakakaa huko wakati mwingi, wakinena kwa ushujaa katika Bwana, aliyelishuhudia neno la neema yake, akiwajalia ishara na maajabu yatendeke kwa mikono yao. Lakini jamii ya watu wa mjini wakafarakana; hawa walikuwa upande wa Wayahudi, na hawa upande wa Mitume. Hata palipotokea shambulio la watu wa Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao, kuwatenda jeuri na kuwapiga kwa mawe, wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia, na nchi zilizo kando kando; wakakaa huko, wakiihubiri Injili.
Matendo 14:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Huko Ikonio Paulo na Barnaba waliingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi kama ilivyokuwa desturi yao. Huko wakahubiri kwa uwezo mkubwa kiasi kwamba Wayahudi pamoja na watu wa Mataifa wakaamini. Lakini wale Wayahudi waliokataa kuamini wakawachochea watu wa Mataifa, wakatia chuki ndani ya mioyo yao dhidi ya waumini. Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri kuhusu Bwana, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza. Lakini watu wa mji ule waligawanyika, wengine wakakubaliana na Wayahudi na wengine na mitume. Watu wa Mataifa na Wayahudi wakajiunga na baadhi ya viongozi, wakafanya mpango wa kuwatendea mitume mabaya na kuwapiga mawe. Lakini mitume walipopata habari hizi wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia na sehemu zilizopakana nayo. Huko wakaendelea kuhubiri Habari Njema.