Matendo 13:24-52
Matendo 13:24-52 Biblia Habari Njema (BHN)
Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa. Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake aliwaambia watu: ‘Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu na mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake.’ “Ndugu, nyinyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi, wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu Yesu adhabu ya kifo. Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe, walimwomba Pilato amhukumu auawe. Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Naye, kwa siku nyingi, aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli. Nasi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: Jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu, amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili: ‘Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.’ Na juu ya kumfufua kutoka kwa wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi: ‘Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi.’ Naam, na katika sehemu nyingine za Zaburi asema: ‘Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.’ Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza matakwa ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza. Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza. Kwa hiyo, jueni, ndugu zangu, kwamba kwa njia ya mtu huyu ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu; na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya sheria. Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii: ‘Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni.’” Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika lile sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee zaidi juu ya mambo hayo. Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu. Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule mji alikuja kusikiliza neno la Bwana. Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana. Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari zaidi, wakasema, “Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni nyinyi kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uhai wa milele, basi, tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine. Maana Bwana alituagiza hivi: ‘Nimekuweka wewe uwe mwanga kwa watu wa mataifa, ili uwaletee watu wokovu pote ulimwenguni.’” Watu wa mataifa mengine waliposikia jambo hilo walifurahi, wakausifu ujumbe wa Mungu; na wale waliokuwa wamechaguliwa kupata uhai wa milele, wakawa waumini. Neno la Bwana likaenea kila mahali katika sehemu ile. Lakini Wayahudi waliwachochea wanawake wa tabaka ya juu wa mataifa mengine ambao walikuwa wacha Mungu, na wanaume maarufu wa mji huo. Wakaanza kuwatesa Paulo na Barnaba, wakawafukuza kutoka katika eneo lao. Basi, mitume wakayakunguta mavumbi yaliyokuwa katika miguu yao kama onyo, kisha wakaenda Ikonio. Lakini hao wafuasi walikuwa wamejaa furaha na Roho Mtakatifu.
Matendo 13:24-52 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiria watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mnadhani mimi ni nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake. Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Abrahamu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumwua wakamwomba Pilato auawe. Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamteremsha kutoka kwa ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hadi Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu. Na sisi tunawahubiria Habari Njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa. Tena ya kuwa alimfufua katika wafu, asipate kurudia uharibifu, amenena hivi, Nitawapa ninyi mambo matakatifu ya Daudi yaliyo amini. Kwa hiyo anena na pengine, Hutamwachia Mtakatifu wako kuona uharibifu. Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu. Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu. Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi; na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa Torati ya Musa. Angalieni, basi, isiwajie habari ile iliyonenwa katika manabii. Tazameni, enyi mnaodharau, kastaajabuni, mkatoweke; kwa kuwa natenda kazi mimi siku zenu, kazi ambayo msingeisadiki kabisa, ijapo mtu akiwasimulia sana. Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya sabato ya pili. Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakawafuata Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu. Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona ninyi wenyewe kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawachochea wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio. Lakini wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.
Matendo 13:24-52 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake. Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe. Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu. Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa. Tena ya kuwa alimfufua katika wafu, asipate kurudia uharibifu, amenena hivi, Nitawapa ninyi mambo matakatifu ya Daudi yaliyo amini. Kwa hiyo anena na pengine, Hutamwachia Mtakatifu wako kuona uharibifu. Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu. Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu. Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi; na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa. Angalieni, basi, isiwajilie habari ile iliyonenwa katika manabii. Tazameni, enyi mnaodharau, kastaajabuni, mkatoweke; kwa kuwa natenda kazi mimi siku zenu, kazi ambayo msingeisadiki kabisa, ijapo mtu akiwasimulia sana. Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya sabato ya pili. Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu. Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung’utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.
Matendo 13:24-52 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kabla ya kuja kwa Yesu, Yohana alihubiri toba na ubatizo kwa watu wote wa Israeli. Yohana alipokuwa anakamilisha kazi yake, alisema: ‘Ninyi mnadhani mimi ni nani? Mimi si yeye. La, lakini yeye yuaja baada yangu, ambaye mimi sistahili kufungua kamba za viatu vya miguu yake.’ “Ndugu zangu, wana wa Abrahamu, nanyi watu wa Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. Kwa sababu watu wa Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua, wala kuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye. Ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe. Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja naye kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu. “Nasi tunawaletea Habari Njema: kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu sasa ameyatimiza kwetu sisi, watoto wao, kwa kumfufua Yesu, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili: “ ‘Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa Baba yako.’ Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya: “ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika nilizomwahidi Daudi.’ Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi, “ ‘Hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.’ “Basi Daudi alipokwisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa na baba zake, na mwili wake ukaoza. Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu. “Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kupitia kwa huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu. Kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Musa. Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate: “ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka, mkastaajabu, mkaangamie, kwa maana nitatenda jambo wakati wenu ambalo hamtasadiki, hata kama mtu akiwaambia.’” Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato iliyofuata. Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na watu wa Mataifa walioongokea dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu. Sabato iliyofuata, karibu watu wote wa mji walikuja kusikiliza neno la Bwana. Lakini Wayahudi walipoona umati ule mkubwa wa watu, walijawa na wivu, wakayakanusha maneno Paulo aliyokuwa akisema. Ndipo Paulo na Barnaba wakawajibu kwa ujasiri, wakisema, “Ilitupasa kunena nanyi neno la Mungu kwanza. Lakini kwa kuwa mmelikataa, mkajihukumu wenyewe kuwa hamstahili uzima wa milele, sasa tunawageukia watu wa Mataifa. Kwa maana hili ndilo Bwana alilotuamuru: “ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu wa Mataifa, ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’” Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika eneo lile lote. Lakini viongozi wa Wayahudi wakawachochea wanawake wenye kumcha Mungu, wenye vyeo pamoja na watu maarufu katika mji, wakachochea mateso dhidi ya Paulo na Barnaba na kuwafukuza kutoka eneo hilo. Hivyo Paulo na Barnaba wakakungʼuta mavumbi ya miguu yao ili kuwapinga, nao wakaenda Ikonio. Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho Mtakatifu.