Matendo 10:9-16
Matendo 10:9-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali. Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, akaota ndoto. Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne. Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: Wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani. Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!” Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.” Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!” Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni.
Matendo 10:9-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inateremshwa kwa pembe zake nne hadi chini; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Inuka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, La, hasha! Bwana, kwa maana sijawahi kula kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni.
Matendo 10:9-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni.
Matendo 10:9-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku iliyofuata, walipokuwa wanaukaribia mji, yapata saa sita mchana, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama kitambaa kikubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.” Petro akajibu, “La hasha, Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.” Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.” Jambo hili lilitokea mara tatu, na ghafula kile kitambaa kikarudishwa mbinguni.