Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 10:1-18

Matendo 10:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho “Kikosi cha Italia.” Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima. Yapata saa tisa alasiri, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, “Kuna nini Mheshimiwa?” Huyo malaika akamwambia, “Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini wala hatazisahau. Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro. Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari.” Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu, akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa. Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali. Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, akaota ndoto. Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne. Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: Wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani. Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!” Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.” Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!” Jambo hili lilifanyika mara tatu, kisha ile shuka ikarudishwa juu mbinguni. Petro alipokuwa bado anashangaa juu ya maana ya hayo maono aliyokuwa ameyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, baada ya kuigundua nyumba ya Simoni, walifika mlangoni, wakaita kwa sauti: “Je, kuna mgeni humu aitwaye Simoni Petro?”

Shirikisha
Soma Matendo 10

Matendo 10:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, jemadari wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamkodolea macho, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, tuma watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda. Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa kati ya wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa. Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inateremshwa kwa pembe zake nne hadi chini; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Inuka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, La, hasha! Bwana, kwa maana sijawahi kula kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. Wakati Petro alipokuwa akisumbuka ndani ya nafsi yake, juu ya maana ya maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakatokeza. Walikuwa kukiulizia nyumba ya Simoni, wakiwa wamesimama mbele ya lango, wakaita; wakauliza kama Simoni aitwaye Petro anakaa humo.

Shirikisha
Soma Matendo 10

Matendo 10:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda. Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa. Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana; akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni. Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango, wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.

Shirikisha
Soma Matendo 10

Matendo 10:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu aliyeitwa Kornelio, aliyekuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. Yeye na jamaa yake yote walikuwa wacha Mungu; alitoa kwa ukarimu kwa wale walio na mahitaji na kumwomba Mungu mara kwa mara. Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!” Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?” Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro. Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.” Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia. Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa. Siku iliyofuata, walipokuwa wanaukaribia mji, yapata saa sita mchana, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama kitambaa kikubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.” Petro akajibu, “La hasha, Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.” Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.” Jambo hili lilitokea mara tatu, na ghafula kile kitambaa kikarudishwa mbinguni. Petro alipokuwa akisumbuka kuhusu maana ya maono hayo, wale watu waliotumwa na Kornelio waliipata nyumba ya Simoni, wakasimama kwenye lango. Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.

Shirikisha
Soma Matendo 10