Matendo 1:1-26
Matendo 1:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. Kwa muda wa siku arubaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu. Wakati alipokutana pamoja nao aliwaamuru hivi: “Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeni ile zawadi aliyoahidi Baba, ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake. Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, nyinyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.” Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, “Je, Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?” Lakini Yesu akawaambia, “Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini. Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni nyinyi, mtapokea nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia.” Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena. Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao, wakasema, “Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mlivyomwona akienda mbinguni.” Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka ule mlima uitwao Mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini. Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake. Siku moja baadaye, Petro alisimama kati ya wale ndugu waumini ambao walikuwa wamekusanyika, wote jumla watu 120, akasema, “Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni. Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu, maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu.” ( Yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu, akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje. Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba “Akel Dama,” maana yake, “Shamba la Damu.”) “Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi: ‘Makao yake yabaki mahame; mtu yeyote asiishi ndani yake.’ Tena imeandikwa: ‘Mtu mwingine achukue nafasi yake ya huduma.’ Basi, mtu mmoja miongoni mwa wale walioandamana nasi muda wote Bwana Yesu alipokuwa anasafiri pamoja nasi achaguliwe kujiunga nasi. Huyo anapaswa kuwa mmoja wa wale walioandamana nasi tangu Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni. Huyo atashiriki pamoja nasi jukumu la kushuhudia ufufuo wake Yesu.” Hapo, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia. Kisha wakasali: “Bwana, wewe unaijua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuoneshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe.” Wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.
Matendo 1:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kitabu kile cha kwanza nilikiandika, Theofilo, kuhusu mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, hadi siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliojidhihirisha kwao kuwa yu hai, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, akiwatokea muda wa siku arubaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Wakati alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kutoka kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na kote katika Yudea, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni. Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato. Wakati walipoingia, wakapanda ghorofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake. Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilikuwa mia moja na ishirini), akasema, Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu; kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. (Basi mtu huyu alinunua shamba kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka. Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata shamba lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, shamba la damu.) Kwa maana imeandikwa katika kitabu cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena, Usimamizi wake autwae mwingine. Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuoneshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.
Matendo 1:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu; ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache. Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi. Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni. Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato. Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake. Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema, Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu; kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. (Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka. Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.) Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena, Usimamizi wake autwae mwingine. Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.
Matendo 1:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyoyafanya na kufundisha tangu mwanzo, hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. Baada ya mateso yake, alijionesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu ufalme wa Mungu. Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.” Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?” Yesu akawaambia, “Sio wajibu wenu kujua nyakati au majira ambayo Baba ameyaweka kwa mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, Roho Mtakatifu akiwajilia juu yenu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na Yudea yote, na Samaria, na miisho ya dunia.” Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena. Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake mbinguni, ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao. Wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni, atarudi tena jinsi hiyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.” Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato kutoka mjini. Walipowasili mjini Yerusalemu, walienda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo na Andrea; Filipo na Tomaso; Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pia walikuwepo wanawake kadhaa, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake Yesu. Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao walikuwa watu wapatao mia moja na ishirini), akasema, “Ndugu zangu, ilibidi andiko litimie, ambalo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda, aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu. Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.” (Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje. Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu.) “Kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Zaburi, “ ‘Mahali pake na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’ na, “ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’ Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiishi kati yetu, kuanzia ubatizo wa Yohana hadi siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.” Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yusufu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, “Bwana, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuoneshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua ili achukue nafasi ya huduma ya utume, ambayo Yuda aliiacha ili aende anapostahili.” Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.