Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Timotheo 2:1-15

2 Timotheo 2:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata katika kuungana na Kristo Yesu. Chukua yale mafundisho uliyonisikia nikitangaza mbele ya mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu wanaoaminika, ambao wataweza kuwafundisha wengine pia. Shiriki katika mateso kama askari mwaminifu wa Kristo Yesu. Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya kawaida, ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi. Mwanariadha yeyote hawezi kushinda na kupata zawadi ya ushindi kama asipozitii sheria za michezo. Mkulima ambaye amefanya kazi ngumu anastahili kupata sehemu ya kwanza ya mavuno. Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha uelewe kila kitu. Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri, na ambayo kwa sababu yake mimi nateseka na nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo. Kwa hiyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao huleta utukufu wa milele. Usemi huu ni wa kweli: “Ikiwa tulikufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye. Tukiendelea kuvumilia, tutatawala pia pamoja naye. Tukimkana, naye pia atatukana. Tukikosa kuwa waaminifu, yeye hubaki mwaminifu daima, maana yeye hawezi kujikana mwenyewe.” Basi, wakumbushe watu wako mambo haya na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia. Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli.

2 Timotheo 2:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu. Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha wengine vile vile. Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu. Askari aliye vitani hajiingizi katika shughuli za dunia, maana lengo lake ni kumpendeza yeye aliyemweka kuwa askari. Hata mwanariadha hapewi taji, asiposhindana kwa kufuata sheria. Yampasa mkulima mwenye bidii ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la mavuno. Yatafakari sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa ufahamu katika mambo yote. Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo Injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wanaoyasikia. Jitahidi kujionesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mfanyakazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.

2 Timotheo 2:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu. Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine. Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu. Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari. Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali. Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda. Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote. Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao. Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.

2 Timotheo 2:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Kristo Yesu. Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile. Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu. Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari. Vivyo hivyo, mwanariadha hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano. Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno. Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Bwana atakupa ufahamu katika mambo haya yote. Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Hili ni neno la kuaminiwa: Kama tumekufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye. Kama tukistahimili, pia tutatawala pamoja naye. Kama tukimkana, naye atatukana. Tusipoaminika, yeye hudumu akiwa mwaminifu, kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. Endelea kuwakumbusha mambo haya, ukiwaonya mbele za Mungu waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote, bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia. Jitahidi kujionesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli.