2 Timotheo 1:7-10
2 Timotheo 1:7-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu. Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unayopewa na Mungu. Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya mastahili ya matendo yetu, bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo kwa ajili ya Kristo Yesu kabla ya wakati, lakini imefunuliwa kwetu sasa kwa kuja kwake Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uhai usio na kifo.
2 Timotheo 1:7-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa uweza wa Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake mwenyewe na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu kabla ya wakati kuanza, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutoharibika, kwa ile Injili
2 Timotheo 1:7-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili
2 Timotheo 1:7-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Maana Mungu hakutupatia roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi. Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema, bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele. Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kupitia kwa Injili.