2 Timotheo 1:1-8
2 Timotheo 1:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo Yesu ili niutangaze ule uhai tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu, nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu. Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka katika sala zangu usiku na mchana. Nakumbuka machozi yako na ninatamani sana kukuona, ili nijazwe furaha. Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo. Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu. Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu. Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unayopewa na Mungu.
2 Timotheo 1:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu; kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nikiyakumbuka machozi yako, natamani sana kukuona, ili nijawe na furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika nyanya yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa uweza wa Mungu
2 Timotheo 1:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu; kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu
2 Timotheo 1:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Paulo mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima ulio ndani ya Kristo Yesu. Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema, rehema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba, na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha. Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike, na ninasadiki sasa wewe pia unayo. Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. Maana Mungu hakutupatia roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi. Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu